Diwani wa CHADEMA aishinikiza Serikali kuanza upya mchakato wa uchaguzi Serikali za Mitaa

0
22Na. John Walter-Manyara

Diwani wa Kata ya Babati mjini (CHADEMA), Mohammed Kibiki ameitaka Serikali ifikirie upya kujiengua kwa vyama vya upinzani kugombea nafasi mbalimbali katika  uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Akizungumza na Muungwana Blog Diwani huyo amesema ikiwezekana serikali irejee upya mchakato wa kuchukua fomu na endapo  ikishindikana basi itoe tamko la kuwarejesha wote waliotolewa bila kujali sababu zilizoelezwa awali kwenye fomu  ili waweze kugombea wananchi waamue wenyewe ni watu gani wanafaa kuwa viongozi na sio vinginevyo.

Kibiki ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata hiyo alisema mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa uligubikwa na changamoto nyingi  zilizosababishwa na wasimamizi wa uchaguzi katika suala la kuchukua fomu na kurudisha fomu.

“Wasimamizi walitoa ushirikiano kwa wao kuwepo katika vituo  walivyopangiwa kwa zile siku 7, lakini hawakutimiza wajibu wao kikamilifu kwa kuwa wao wanauelewa mkubwa kuliko wagombea watarajiwa kwa sababu mgombea anapochukua fomu na kurudisha, msimamizi wa uchaguzi anapaswa kuhakiki fomu, kwani katika nchi yetu mwalimu nyerere alituachia ujinga kwa asilimia 80% katika suala zima la elimu ingawa kwa sasa inaelekea kushuka kwa hiyo anapaswa kuambiwa amekosea wapi kwani hata wabunge na madiwani huwa wanakosea wakati wa kujaza fomu na tunaambiwa lakini katika uchaguzi huu umekuwa kama mtego”alisema Kibiki.

Amesema wagombea watatu  walioteuliwa kwenye nafasi ya kugombea uwenyekiti walifanyiwa hujuma na kutenguliwa nafasi hizo.

 “Kulikuwa na nia ovu ya chama Tawala  kwa kushirikiana na serikali  ya chama cha Mapinduzi  kuhakikisha kwamba wagombea wa upinzani wote wanaenguliwa katika kupewa nafasi ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,hivyo nampongeza mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo Taifa,Freeman Mbowe  kwa kuamua kutoshiriki uchaguzi huo,  amefanya maamuzi sahihi kupitia kamati kuu kutoshiriki uchaguzi, pia nawaunga mkono ACT Wazalendo kwa kujitoa katika uchaguzi” alisema  kibiki

Naye Mariam Athumani  Ally mkazi wa mtaa wa Babati mjini  ambaye alikuwa mgombea nafasi ya wa Mwenyekiti wa mtaa huo kupitia CHADEMA ameeleza kwamba katika mchakato uliokuwa umefanyika wa kuchukua fomu na kurejesha fomu hawakutendewa haki.