Rais Tshisekedi akutana na Museveni Kampala

0
13

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yuko nchini Uganda kwa lengo la kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili jirani, hatua ambayo inatekelezwa baada ya Rwanda kuifunga mipaka yake kwa Uganda.

Baada ya kukutana na kiongozi wa Congo mjini Kampala, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema mataifa hayo mawili yatajenga ushirikiano madhubuti.

Aliongeza kusema kuwa watajenga barabara na madaraja yatakayounganisha mataifa hayo mawili, akisisitiza kuwa hatua hiyo ina shabaha za kibiashara, ustawi wa jamii na ulinzi.

Biashara kati ya mataifa hayo mawili kwa mwaka uliopita ilifikia thamani ya dola milioni 513, lakini kwa sasa kuna ishara ya kuongezeka, baada ya Uganda kuelekeza zingatio lake nchini Congo, hatua inayotokana na Rwanda kuufunga mpaka wake Februari.

Museveni na Tshisdekedi wamekubaliana kujenga barabara ya umbali wa kilometa 1,200 kuanzia Uganda kuelekea katika miji mitatu ya eneo la mashariki mwa Kongo ya Goma, Bunia na Beni.