Tanzania yapunguza maambukizi ya Malaria kwa asilimia 50

0
6

Serikili kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kupunguza maambukizi ya malaria kwa takribani asilimia 50% kutoka 14.8% mwaka 2015 mpaka kufikia 7.3% mwaka 2017.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wakiongozana na Mawaziri kutoka nchi za SADC ziarani Mkoa wa Pwani, Kibaha walipotembelea Kiwanda cha Viuadudu wa kibaiolojia cha TBPL.

Waziri Ummy Mwalimu amesema, mafanikio haya ni kutokana na kuwekeza rasilimali fedha, utashi wa viongozi, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla katika kutekeleza mikakati ya udhibiti wa malaria.

Mojawapo ya afua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kudhibiti ugonjwa wa malaria ni kujenga kiwanda cha viuadudu vya kibailojia kwa ajili ya kuua mazalia, alibainisha Waziri Ummy.

Aliendelea kusisitiza kuwa matumizi ya viuadudu hivyo vya kibailojia ni kwa ajili ya kuangamiza viluilui vya mbu wanavyoeneza magonjwa mbalimbali yakiwemo; malaria, homa ya dengue, zika, homa ya manjano, matende, giri-majihoma ya bonde la ufa na chikungunya.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa ili kuendeleza mafanikio na hatimae kutokomeza kabisa malaria katika nchi zote za SADC tunahitaji kuongeza wigo na kuhakikisha nchi wanachama wanaongeza rasilimali fedha ili kutekeleza afua mbalimbali za udhibti wa malaria, alisema.