Wasichana watano kuuwakilisha mkoa wa Manyara Mashindano ya riadha Taifa

0
19Na John Walter-Manyara

Afisa  Michezo wa mkoa wa Manyara Charles Maguzu, ameomba wazazi na walezi kuwahimiza watoto wao kushiriki katika mchezo wa riadha.

Ametoa wito huo wakati akishudia mchujo wa kuwapata wanariadha wa kike watano watakaouwakilisha mkoa wa Manyara kwenye mashindano ya Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam na baadaye nchini Japan.

Akizungumza na Muungwana Blog Maguzu amesema wasichana waliojitokeza katika kuwania mbio za kushiriki riadha Kitaifa ni wachache, hivyo wazazi wajitahidi kuhimiza watoto wao wajiunge kwenye mchezo huo ambao umewainua wengi kiuchumi na kuutangaza mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla.

Wasichana watano waliopatikana ni wa mbio za mita 5,000 Loema Awaki kutoka Mbulu, na Paulina Stephano wa wilaya ya Hanang,Mita 1,500 Oliva Francis wa Mbulu na Yusta Ninga kutoka Babati, wakati watakaoshiriki Mita 800 ni Neema Sanka.

“Baada ya kupatikana timu ya wanariadha ya wanawake, bado wanahitaji sapoti ya mashindano mbalimbali kwa ajili ya kujiandaa vyema, hivyo wadhamini wanahitajika katika hilo,” alisema.

Alisema Wanariadha hao watawasili Dar es Salaam Desemba 5 na kwa ajili ya kujiandaa na mashindano Desemba 7 na wanatarajiwa kurejea Manyara Desemba 9 mwaka huu.

Kila la kheri kwa wote waliochaguliwa kuuwakilisha mkoa wa Manyara katika mashindano hayo,Mungu Ibariki Manyara,Mungu ibariki Tanzania.