Afrika Kusini: Watu wanne wahofiwa kufa baada ya kunasa chini ya mgodi

0
17

Kuna hofu kuhusu uhai wa raia wanne wa Afrika Kusini, wachimbaji walionasa ardhini baada ya tetemeko lililosababisha kuanguka kwa mwamba.

Advertisement

Siku ya Ijumaa mtu wa tano aliokolewa kutoka kwenye mgodi wa Tau Lekoa ulio Kusini Magharibi mwa mji wa Johnnesurg.

Umoja wa wafanyakazi wa migodi nchini humo umesema kikosi cha uokoaji kimepoteza mawasiliano na watu wanne walionasa. Wako umbali wa kilomita kadhaa ardhini ambapo mfumo wa hewa ni hafifu na joto ni kali sana.

Ujumbe wa mwisho walioutuma ni ombi lao kupatiwa hewa ya oksijeni. Lakini kutokana na hali ilivyo ya hatari katika mgodi wa dhahabu maafisa wamesema itawachukua siku kadhaa kuwafikia.

Serikali ya Afrika Kusini imekuwa katika shinikizo la kuhakikisha kuwa kunakuwa na mazingira salama kwa wachimbaji.

Hali sasa imeimarika – kuna ajali chache. Lakini mashirika ya wafanyakazi wanasema bado hali ni mbaya. Mwaka jana watu 81 walipoteza maisha kwenye migodi nchini humo.

Mwanzoni mwa mwaka jana mamia ya wachimba migodi walikwama katika mgodi mmoja wa dhahabu ulioko eneo la mkoa wa Free State nchini Afrika Kusini.

Kikosi cha uokoaji katika kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Sibanye kilisema zaidi ya wachimba migodi 950 walikwama chini ya mgodi wa dhahabu wa Beatrix ulioko mkoa wa Free State kilomita 300 Kusini Magharibi mwa Johannesburg.

Chanzo cha wachimba migodi hao kukwama ilikuwa radi kubwa iliyopiga na umeme baada ya mvua kubwa kunyesha nyakati za usiku wakati wachimba migodi hao walipokua chini ya mgodi huo.

Maelfu ya wachimba migodi wasio na vibali hufanya kazi kwenye migodi mingi ya dhahabu, maeneo yanayozunguka mji wa Johannesburg.Facebook Comments