Haki kwa walemavu zimeanza kuonekana – Mwenyekiti wa walemavu

0
7

Na Amiri kilagalila-Njombe

Haki na usawa kwa  watu wenye ulemavu mkoani Njombe kusini mwa nchi ya Tanzania zimeanza kuonekana kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na kuongezeka kwa uelewa kwa jamii ya wakazi wa mkoa wa Njombe

Miongoni mwa haki ambazo zinaonekana kutekelezwa kwa walemavu wa mkoa wa Njombe ni pamoja na haki ya kupata elimu,haki ya kusikilizwa pamoja na kupata huduma katika ofisi za serikali na sekta binafsi.

Nickson Muhogofi ni mwenyekiti wa vijana wenye ulemavu mkoani Njombe anayekabiliwa na changamoto ya ulemavu wa macho,anasema kwa sasa jamii imeanza kuwa na mtazamo chanya dhidi ya walemavu tofauti na ilivyokuwa awali.

“Kimsingi kwa saizi katika maswala ya haki tumeanza kusogea baada ya serikali na sisi wenyewe kupiga kelele lakini mwanzo hatukuwa vizuri kwasababu jamii ilikuwa na mtazamo hasi na sasa hivi wakati mwingine haki za watu wenye ulemavu zimeanza kuonekana mfano katika elimu kwa mkoa wa Njombe tuna shule 6 zinachukua watu wenye ulemavu”alisema Nickson Mhogofi

Aidha amesema bado maisha kwa watu wenye ulemavu kwa mkoa wa Njombe ni duni na kuishukuru serikali kwa kuendelea kutenga asilimia katika halmashauri kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Njombe akiwemo Odama Hongoli anasema bado katika jamii kuna dhana potofu dhidi ya walemavu hususani katika swala la ajira.

“Ajira ni ngumu sana kwa walemavu mtu akishaona mtu mlemavu hawezi kumpa ajira kwasababu anaona mlemavu kwa kuwa haamini kama anaweza kufanya kazi lakini mimi naona mlemavu anaweza kufanya kazi vizuri kuliko mwenye viungo vyote kwa kuwa ni lazima atakuwa makini zaidi ya asiyekuwa mlemavu”alisema Odama Hongoli

Disemba tatu ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya walemavu ambapo baadhi ya walemavu mkoani Njombe waliozungumza na Muungwana blogu wametoa rai kwa jamii kuendelea kubadilika na kuwa na mtazamo chanya dhidi yao.

Aidha disemba tatu mwaka 2018 umoja wa mataifa ulizindua ripoti yake ya  kwanza kuhusu ulemavu na maendeleo ambayo ilitolewa na kuchapishwa na watu wenye ulemavu kwa ajili ya kundi hilo kwa matumaini ya kuchagiza fursa zaidi na kuwa na jamii jumishi zisizowaacha nyuma watu wenye ulemavu.