Jinsi ya kuweza kupata wazo la kufanya biashara nzuri

0
11

Je
nifanye biashara gani? Hilo ni moja ya swali ambalo nimekuwa nikiulizwa
mara kwa mara na wajasiriamali  wakiwamo wale wanaohitaji kuanzisha
aina nyingine ya biashara.
Kimsingi kuna mamilioni ya
wajasiriamali ulimwenguni ambao baadhi wamebainisha kwamba vyanzo vikuu
vya kupata wazo zuri la biashara ni kama ifuatavyo. 

Kitu ukipendacho sana (hobby)
Mara
nyingi watu hupenda kutumia muda fulani katika siku ama wiki
kujiburudisha na vitu wavipendavyo mathalani kuchezea kompyuta, kupika,
muziki, safari, michezo, na kufanya  mazoezi.
Kutokana na kufanya
jambo unalolipenda unaweza kuibua wazo la biashara, mathalani kuna watu
wanapenda kunywa vilevi na mwisho wa siku wananzisha biashara ya baa.

Wengi
wanafanya hivyo kutokana na mtandao mkubwa waliojijengea na kufanikiwa
kupata wateja wengi na biashara kwenda vizuri. Kwa upande mwingine watu
wanaopenda muziki huweza kubadili mapenzi hayo ya muziki na kufanya
shughuli za kimuziki kibiashara.

Ujuzi na uzoefu
Tafiti
nyingi zinaonyesha biashara zilizofanikiwa zimetokana na ujuzi na
uzoefu wa mwanzilishi, mathalani mtu aliyeajiriwa kama mhasibu anaweza
baadaye akafungua biashara ya mambo ya ukaguzi wa mahesabu, daktari
anaweza kuanzisha biashara ya afya (kituo cha afya hadi hospitali) na
askari anaweza kufanya biashara ya ulinzi.

Kutokana na hali hiyo tunajifunza  ujuzi na uzoefu unasaidia kuamua kuamua aina gani ya biashara ufanye.

Matumizi ya haki miliki
Kuna
biashara ambazo zinafanya vizuri sokoni na kwa kuwa zimesajiliwa
kisheria zinahaki miliki husika. Kwa mfano, wewe badala ya kufikiria
kuanzisha biashara gani unaweza kuingia mkataba na mmiliki wa biashara
hiyo ili uzalishe bidhaa ama utoe huduma kwa jina la biashara yake na
kwa viwango anavyotumia ilimradi ulipie gharama ya tozo kwa kutumia hati
miliki yake.

Vyombo vya habari
Vyombo vya
habari ni hanzo kikubwa sana cha habari na taarifa kinachoweza kukupa
wazo zuri na fursa mbalimbali za kibiashara. Vyombo vya habari vyaweza
kuhusisha magazeti, runinga na siku hizi mitandao ya kijamii.

Kwa
mfano unaweza kusoma au kuona habari kuhusu biashara fulani inauzwa na
wewe mara moja baada ya kuiona biashara hiyo unashawishika kuinunua.
Habari kwenye vyombo vya habari zinahusu mambo mengi ya kijamii,
kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia, hivyo unapozipata ni rahisi kugundua
fursa za kibiashara.

Maonyesho
Maonyesho ya
kibiashara ni sehemu muhimu sana inayokutanisha wagavi, watengenezaji
wa bidhaa mbalimbali, wanunuzi na wasambazaji. Kuhudhuria maonyesho ya
biashara ambayo mara nyingi yanatangazwa kwenye vyombo vya habari
itakusaidia   kujifunza mengi kutoka kwa watu wengine na kuvutiwa na
biashara ambayo unaweza kuifanya.

Tafiti
Tafiti
ni suala pana sana ila, unaweza kufanya kwa namna unavyoweza wewe,
mathalani unaweza kuwa na mawazo mengi ya biashara na hujafikia uamuzi
wa biashara ipi ufanye.

Kwanza unapaswa kupanga mawazo ya biashara
kuendana na kipaumbele na ukibakia na mawazo matatu, jaribu kuuliza
kuuliza watu mbalimbali wakiwamo wateja na watu wanaofanya biashara kama
hiyo. Kwa mfano zungumza na watu wanakwenda safari ndefu kufuata bidhaa
za majumbani kwa jumla, ni rahisi kwako kuanzisha biashara ili
uwapunguzie adha watu wa eneo hilo.

Malalamiko
Tumia
malalamiko kama njia ya kupata wazo la kuanzisha biashara mpya. Mara
nyingi tumekuwa tukishuhudia foleni kubwa kwenye benki, kucheleweshewa
mkopo, magari ya abiria kujaza sana na vikwazo vingine vingi, katika
hili pia unaweza kupunguza malalamiko hayo kwa kuanzisha biashara mpya.

Kwa
mfano, nina rafiki yangu alisajili kampuni ya kukopesha baada ya
kucheleweshewa mkopo benki kwa miezi sita. Kampuni yake inatoa mkopo
ndani ya muda mfupi sana ukilinganisha na benki.