Katibu Mkuu Nishati akagua mitambo ya Gesi Songongo na Mnazi Bay

0
10

Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, amefanya ziara ya kikazi katika mitambo ya kuzalisha, kuchakata na kusafirisha Gesi Asilia iliyopo kisiwani Songo Songo mkoani Lindi, na ile ya Madimba na Mnazi Bay Mkoani Mtwara kwa lengo la kukagua maendeleo ya uzalishaji na uchakataji wa Gesi Asilia katika maeneo hayo.

Ziara hiyo aliifanya Disemba 11, 2019 akiwa ameambatana na Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi, Kamishna Msaidizi wa Gesi, Sebastian Shana na watendaji kutoka kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ya GASCO inayoshughulikia masuala ya Usambazaji Gesi.

Advertisement

Pamoja na  ukaguzi wa maendeleo ya uzalishaji na uchakataji wa Gesi Asilia katika maeneo hayo, ziara hiyo ililenga kubaini kama kuna changamoto ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Gesi Asilia nchini.

Baada ya ukaguzi wa mitambo hiyo, Katibu Mkuu aliwapongeza watendaji wa TPDC na GASCO kwa jinsi walivyoweza kujenga uwezo kwa maafisa wake ambao ndio wanaendesha mitambo hiyo ya  kuchakata Gesi Asilia bila kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi.

Vile vile, aliwaagiza wataalam hao kusimamia vizuri mitambo hiyo ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa Gesi Asilia ambayo inatumika kwa matumizi mbalimbali nchini ikiwemo kuzalisha umeme, kutumika majumbani, viwandani na kwenye magari.


Facebook Comments