Maafisa Michezo lindeni viwanja vya Michezo nchini – Dkt. Mwakyembe

0
19

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka Maafisa Michezo kote nchini  kulinda viwanja vya michezo na kutoa taarifa ya viwanja vya michezo vinavyobadilishwa matumizi hata kwa siri.

Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Michezo kinachofanyiki kwa siku mbili chenye lengo la kutathimini, kujadili na kuelekezana namna bora ya kuimarisha michezo na kutumia sekta hiyo kutangaza vivutio vya utalii nchini.

Advertisement

“Wapo baadhi ya Wakuu wa shule na walimu wanaozuia michezo shuleni na mnawajua, mnakaa kimya sasa wajibu wenu ni nini? Tambueni michezo sasa ni ajira ambayo ni mgodi na taifa lina vijana wengi simamieni vyema michezo,” Dkt. Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza katika ufunguzi wa kikao kazi hicho Dkt. Mwakyembe amekiagiza Chuo cha Michezo cha Malya kufanya utafiti wa kodi inayotokana na michezo mbalimbali inayofanyika nchini.

Naye Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo kukakikisha kikao kazi hicho kinakuwa endelevu na kufanyika kila mwaka. Aidha, aandae utaratibu wa kuwa na vikao hivyo kikanda vikiwa na lengo la kuwaandaa vijana waweze kushiriki michezo mbalimbali kitaifa na kimataifa.

“Kikao Kazi hiki kitatoa tathimini ya wapi tulipo, nini kifanyike pamoja na kutoa mwongozo wa kusimamia michezo mbalimbali na kutoa maelekezo kwa kuweka maazimio yatakayosaidia kupeleka michezo kuwanufaisha vijana maana michezo ni ajira,” alisema Dkt. Possi.

Aidha, Dkt. Possi aliwataka maafisa michezo hao kuzingatia mada ya uandishi wa maandiko ya udhamini katika michezo ambayo ni kichocheo cha kufanikisha michezo nchini kwani maandiko mradi hufanyika ni miongoni mwa kazi inayofanyika kila siku katika sekta ya michezo, hivyo ni  vyema kuwa na ujuzi huo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo alitoa pongezi na shukrani kwa Makatibu Tawala Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri kwa kuwawezesha maafisa michezo hao kushiriki kikao hicho kwa mikoa yote nchini imeshiriki.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho Afisa Michezo kutoka Wilaya ya Mbarali Bw. Gerald Chiwaya aliishukuru wizara kwa kuandaa kikao hicho ambacho kimefanyika kwa mara ya kwanza nchini ambacho kina washiriki 265 kutoka mikoa yote Tanzania Bara.


Facebook Comments