Makosa 8 ya kuepuka kabla na wakati wa kujenga nyumba

0
16

Nyumba Nzuri

Nyumba
ni hitaji muhimu kwa watu wote. Kila mmoja anatamani na ana ndoto za
kununua au kujenga nyumba nzuri na ya kisasa. Ni kweli kuwa ujenzi wa
nyumba unahitaji rasilimali nyingi hasa fedha.

Pamoja na gharama
hizi za ujenzi wa nyumba bado watu wengi wamekuwa wakishindwa kupata
nyumba nzuri huku wakiwa tayari wamepoteza kiasi kikubwa cha pesa. Ni
wazi kuwa yapo makosa mbalimbali yanayosababisha hali hii yakiwemo yale
ya ukosefu wa elimu pamoja na uzembe wa aina mbalimbali.

Karibu
ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu makosa 8 unayoweza kuyaepuka
wakati wa kujenga nyumba ili hatimaye uwe na nyumba bora.

1. Kutozingatia kanuni za kununua kiwanja

Watu
wengi hawafahamu mambo muhimu ya kuzingatia wakati wanaponunua kiwanja.
Hivyo hujikuta wakiingia katika matatizo mbalimbali kama vile kuvunjiwa
nyumba zao, kujenga kwenye maeneo mabaya kama matindiga na mikondo ya
maji. Ni muhimu kuhakikisha mambo yafuatayo kabla na wakati wa kutafuta
kiwanja cha kujenga nyumba:

 • Kiwanja hakina umiliki zaidi ya mtu mmoja
 • Kiwanja hakina mgogoro wa kisheria
 • Kiwanja hakiko kwenye hifadhi ya barabara au mazingira
 • Kiwanja kinafaa kwa ujenzi (Siyo tindiga, eneo la magadi, eneo la maporomoko ya ardhi au mkondo wa maji)

Ukizingatia haya utaweza kupata kiwanja kizuri kwa ajili ya kujenga nyumba bora kwa ajili ya matumizi yako.

2. Uchaguzi duni wa ramani

Mara
nyingi mtu humwita fundi na kumwambia kuwa “nataka unijengee nyumba ya
vyumba vitatu”. Fundi anapouliza ramani yako iko wapi wao husema we
angalia tu nzuri alimradi iwe ya vyumba vitatu. Hili ni kosa kubwa sana
kwani husababisha watu wengi kujengewa nyumba ambazo hawazipendi.
Ramani
nzuri kwa fundi inaweza isiwe nzuri kwako na familia yako. Zingatia
uchaguzi wa ramani kwa makini kulingana na wewe unavyopenda, hili
litakufanya pia upende nyumba itakayojengwa.

Ramani
Ramani mbaya.

3. Kutokufanya makadirio sahihi

Ni
wazi kuwa umeona nyumba nyingi zikianzwa lakini hazimaliziki. Hili kwa
kiasi kikubwa linatokana na kufanya makadirio na maandalizi duni kabla
ya kuanza kujenga. Ujenzi wa nyumba unahitaji maandalizi mazuri hasa
kifedha. Ni muhimu kujiandaa vyema kabla ya kuanza ujenzi ili usikwamie
njiani.
Mambo unayoweza kufanya:

 • Weka makadirio ya gharama za ujenzi ili angalau uandae kiasi fulani cha pesa.
 • Nunua
  baadhi ya vifaa kabla. Unaweza kununua mchanga, mawe, kokoto, nondo,
  mabati n.k. Ili kupunguza matumizi ya pesa wakati wa ujenzi.
 • Weka
  mipango ya kutunza mahitaji yako mengine ya pesa kabla ya kuanza
  ujenzi. Kwa mfano ada za shule, kodi mbalimbali, chakula n.k.
 • Punguza matumizi yasiyokuwa ya lazima kabla na wakati wa ujenzi. Ikumbukwe kuwa pesa nyingi zitahitajika kwenye ujenzi.

4. Kutokubainisha mahitaji

Mahitaji
ya nyumba hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Hivyo ni vyema
ukabainisha mahitaji yako kwa nyumba husika. Nimeshuhudia watu wakijenga
nyumba na kuzivunja ua kuzifanyia marekebisho kila mwaka kutokana na
kutobainisha mahitaji yao mapema.
Kurekebisha au kuvunja na
kujenga upya nyumba yako kutakupotezea kiasi kikubwa sana cha pesa. Kwa
mfano wengi hurekebisha nyumba zao ili kuongeza vitu kama vile jiko,
choo na bafu, milango, madirisha n.k. ambavyo wangepanga mapema
wangekuwa wameviweka mwanzoni.

5. Kutokuwaza mbeleni

Ni
vyema kuwaza mbeleni kwani nyumba ni kitu utakachokitumia muda mrefu. Ni
vyema ukafahamu vitu na mahitaji utakayoyataka kwenye nyumba yako kwa
siku za mbeleni. Hili litakuwezesha kujenga nyumba utakayoitumia na
kuifurahia kwa muda mrefu zaidi.
Ni vyema pia ukawaza kuweka
miundombinu ya kisasa kama vile umeme, simu (intercom), nyaya za
televisheni, Kiyoyozi, na hata Data. Hata kama huna pesa za kuweka mambo
haya unaweza kubuni nyumba ambayo baadaye itaruhusu miundombinu hii.

Nyumba
 
Nyumba ya Kisasa

6. Kutumia mafundi duni

Wengi
hupenda kuokoa gharama kwa kutumia mafundi wenye uwezo mdogo ili
wawalipe kwa bei nafuu. Ni wazi kuwa rahisi inaumiza. Jiande vyema kabla
ya ujenzi ili uweze kuitendea haki nyumba yako kwa kutumia mafundi bora
wanaoimudu kazi yao vyema. Kutumia mafundi bora kutakufanya kupata pia
kazi yenye ubora.

Nhazi
Ngazi zilizokosewa.

7. Kupuuza kanuni muhimu za ujenzi

Ujenzi
una kanuni zake mbalimbali ambazo ni vyema zikazingatiwa. Kutokana na
uelewa mdogo, watu wengi hawazingatii kanuni muhimu za ujenzi kama vile
kumwagilia maji yakutosha pamoja na kujenga nyumba kulingana na muda.
Nimeshuhudia
nyumba nyingi zikivunjika kutokana na kujengwa haraka haraka bila kutoa
muda wa kutosha kwa nyumba kukomaa na kustahimili uzito. Pia nimeona
watu wakipuuzia umuhimu wa kunyesha sehemu iliyojegwa kwa maji mengi; ni
muhimu kunyesha vyema eneo lililojengwa kwani “uimara wa saruji ni
maji”; unaweza kunyesha angalau kwa siku saba asubuhi na jioni.

Nyumba iliyoporomoka
 
Nyumba iliyoporomoka kutokana na kupuuza kanuni za ujenzi.

8. Matumizi ya vifaa duni

Kama
nilivyoeleza katika maelezo yaliyotangulia, uhaba wa fedha huwafanya
watu wengi kufanya kazi duni. Hivi leo kuna vifaa mbalimbali vya ujenzi,
lakini si vyote ni bora. Kwa mfano, hakuna haja ya kununua kitasa
kinachovunjika baada ya mwezi au vigae vinavyofubaa. Kwa kufanya hivi
utapoteza pesa nyingi kwa kununua vifaa hivyo mara kwa mara. Jibane,
jipange ufanye kitu cha uhakika.

Hitimisho

Ni
wazi kuwa ujenzi wa nyumba ni shunguli pevu inayohitaji kutulia, moyo
na maandalizi stahiki. Hakuna kitu kinachoshinda nia na mipango mizuri.
Naamini kwa kuyaepuka makosa tajwa hapo juu utaweza kujenga nyumba bora,
salama na ya kisasa kabisa.
Je umeshajenga nyumba yako?
Ulipata changamoto gani na ulizitatuaje? Tafadhali tushirikishe kwa
kutoa maoni yako hapo chini. Pia usisahau kulike ukurasa wetu wa
Facebook pamoja na kuwashirikisha wengine makala hii.