News Wazazi, Walezi wapunguzieni kazi wanafunzi wa madarasa ya mitihani...

Wazazi, Walezi wapunguzieni kazi wanafunzi wa madarasa ya mitihani – RC Mtaka

-

 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapunguzia kazi  wanafunzi walio katika madarasa ya mitihani ya Taifa (darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne) ambayo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni ili waweze kujipatia muda mwingi wa kujisomea kujiandaa na mitihani hiyo.

Mtaka ameyasema hayo jana  wakati makabidhiano ya Chuo cha Ufundi Kasoli katika Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi kilichojengwa na mwekezaji Alliance Ginnery Limited na kukabidhiwa kwa Serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi kwa niaba ya kampuni hiyo na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa niaba ya wananchi.

“Darasa la saba wameshafanya mtihani wao, watoto wa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne waendelee kufanya maandalizi, wazazi na walezi wapunguzieni kazi watoto wote walio kwenye madarasa haya na wakiwa nyumbani wafanye majadiliano ya pamoja,” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amewaonya wazazi na walezi wenye nia ya kuwaozesha wanafunzi wa kike waliohitimu elimu ya msingi kuwa watakaofanya hivyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, huku akitoa wito kwa jamii yote kuwa walinzi wa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

Mtaka ameishukuru Kampuni ya Allience Ginnery kujenga chuo cha ufundi Kasoli na kutoa wito kwa wasichana na wanawake kijiji cha Kasoli kujitokeza kupata mafunzo ya ushonaji bila malipo katika chuo hicho katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, kabla ya kuanza kwa mafunzo yatakayoanza mwakani kwa mtaala wa Serikali na kuahidi kutoa vyerehani 25.

Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, Bw. Boaz Ogola amesema Kampuni hiyo imekuwa inajihusisha sana na maendeleo ya jamii katika sekta ya elimu, afya na maji kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii, ni wajibu wao  kufanya hivyo na ni sehemu ya maelekezo ya TIC wanayopewa wawekezaji wote.

“Tunashiriki kwenye masuala ya jamii kwa sababu sisi ni sehemu ya jamii, sisi tunashughulika na wakulima na wanaotulimia pamba na kutuuzia kutuwezesha kuendesha kiwanda chetu, siku za nyuma tulijikita kwenye afya, maji na elimu ya msingi na sekondari; tumeona haja ya kujenga chuo cha ufundi ili wanafunzi watakaoshindwa kuendelea na masomo, wapate mafunzo  ya ufundi ili waweze kujitegemea,” alisema Ogola.

Aidha, Ogola amesema pamoja na mafunzo ya ufundi mipango ya baadaye ya kampuni ya Alliance Ginnery kuongeza darasa moja la wakulima kwa lengo la kutoa warsha na mafunzo kwa wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija ili kampuni hiyo iweze kupata malighafi bora kwa ajili ya kiwanda chake cha kuchambua pamba..

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi ameipongeza na kuishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kujenga chuo cha Ufundi na kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi walio katika maeneo yao huku akiahidi kuwa TIC itahakikisha kinakuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji.

 “TIC inashirikiana na Serikali hata ngazi ya mikoa na tumejielekeza zaidi kuongeza ufanisi katika shughuli zetu za kuwasaidia wawekezaji masuala ya vibali kwa kushirikiana na Taasisi zinazohusika; pia tumejipanga hata kuwafikia wawekezaji wadogo Watanzania maana baada ya tathmini tumeona eneo hilo kuna mapungufu maana wengi wanadhani sisi tunahusika na wawekezaji wa kigeni tu,” alisema Dkt. Kazi.

Naye Mkazi wa Kijiji cha Kasoli Shamsa Abdallah amesema anaishukuru Kampuni ya Alliance Ginnery kwa kuwajengea chuo cha ufundi na anaamini kuwa kitawasadia kwenye mafunzo ya ushonaji  na mafunzo yanayohusiana na kilimo yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Kampuni ya Alliance Ginnery Limited imejenga majengo ya chuo cha ufundi Kasoli kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 180, kuchimba kisima cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5000 kwa saa pamoja na kuweka vifaa kama vyerehani, majiko ya gesi  na vifaa mbalimbali vya kujifunzia upishi,vifaa vya kujifunzia uashi na useremala meza na viti vya ofisi.

Publisher
Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

Leave a Reply

Latest news

Jewish Settlers Storm Al-Aqsa Mosque Compound under Israeli Police Protection

- World news -  “Under the protection of Israeli police, over 100 settlers stormed the compound through Al-Mugharbah...

Treasury to Hold NMS Staff Salaries Over Dispute

Treasury CS Ukur Yattani declined a request to release money to pay salaries to the Nairobi Metropolitan Services (NMS) staff,...

South Korea Sticks to Flu Vaccine Plan despite 25 Deaths

- Other Media news - Health authorities said they found no direct links between the deaths and the...

Must read

You might also likeRELATED
Recommended to you