News Vikosi vya Ethiopia vyaelekea mji mkuu wa Tigray

Vikosi vya Ethiopia vyaelekea mji mkuu wa Tigray

-

Jeshi la Ethiopia linasonga mbele kuelekea mji mkuu wa jimbo la Tigray Mekelle. Serikali imesema hayo leo huku waasi wakidai kuwa raia wawili wameuawa kufuatia mashambulizi ya angani katika mji huo. 

Jopo kazi la serikali ambalo linafuatilia machafuko hayo, limesema kwenye taarifa kwamba wakati vikosi vilivyojihami vya serikali vikielekea katika mji wa Mekelle, wapiganaji wa chama tawala katika jimbo hilo; Chama cha Ukombozi wa Watigray-TPLF, wameyavunja madaraja manne katika barabara zote za kuingia katika mji huo.  

Ofisi ya habari na mawasiliano ya serikali ya jimbo la Tigray imesema raia wawili waliuawa siku ya Jumatatu kufuatia mashambulizi ya angani kwenye mji wa Mekelle, madai ambayo serikali kuu imekanusha.  

Ofisi hiyo imeongeza kwamba raia 100,000 wameyapoteza makaazi yao kufuatia mapigano, na wanahitaji msaada wa dharura wa kiutu.  

Tigray ni kama ‘jehanamu’ kwa maadui 

Wakati huo huo, viongozi wa jimbo la Tigray wamesema leo kwamba katu hawatasalimu amri kwa vikosi vya serikali kuu na kwamba hivi karibuni wataishinda operesheni hiyo dhidi yao ambayo sasa imedumu kwa wiki mbili.  

Afisa mmoja wa serikali ya jimbo hilo amesema Tigray sasa ni kama jehanamu kwa maadui.

Hakukuwa na jibu la moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuhusiana na kauli hiyo. Mgogoro kati ya serikali kuu ya Ethiopia na jimbo la Tigray ulianza mapema mwezi huu wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipowapeleka wanajeshi kuzima uasi wa TPLF. 

Chama cha TPLF ambacho ni cha Tigray, kimetawala siasa za Ethiopia kwa muda mrefu. Lakini wakati Abiy Ahmed alipochukua madaraka mwaka 2018, amekuwa na mkwaruzano na viongozi wa jimbo la Tigray, akiwaondoa katika serikali na asasi za serikali. 

Pande zote mbili zimeripoti umwagikaji damu. Lakini suala la intaneti kusuasua pamoja na mawasiliano kwa njia ya simu kuzuiwa imefanya hali kuwa ngumu kufahamu kinaganaga kile kinachoendelea Tigray.  

Mnamo mwisho wa wiki iliyopita, TPLF ilisema ilifyatua makombora kuelekea nchi jirani ya Eritrea, ikidai inashirikiana na serikali ya Ethiopia katika machafuko hayo.  

Hofu ya nchi za kanda kujiingiza kwenye machafuko ya Tigray 

Wachambuzi na waangalizi wanahofia huenda nchi nyingine katika ukanda huo zinaweza kuingilia mzozo huo hali inayoweza kutanua machafuko.  

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo ameshutumu vikali mashambulizi yaliyofanywa na TPLF dhidi ya Eritrea. 

Mnamo siku ya Jumanne, Umoja wa Mataifa ulisema eneo la kaskazini mwa Ethiopia linaelekea kukumbwa na janga kubwa la kibinadamu. Umoja huo uliongeza kuwa maelfu ya raia wamekuwa wakikimbia eneo hilo la Tigray kila siku kwa sababu ya machafuko. 

Umoja huo ulisema takriban Waethiopia 27,000 wamekimbilia Sudan. Idadi ya wakimbizi ikiongezeka hadi 4,000 kila siku.  

Tahadhari hiyo ilijiri mnamo wakati wanadiplomasia na maafisa wa kiutu waliripoti mapigano makali katika jimbo la Tigray, huku vikosi vya serikali vikidai kuyakomboa maeneo kadhaa kuwawezesha kusogea karibu na mji mkuu Mekele. 

Publisher
Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

Leave a Reply

Latest news

Palestine teachers begin strike over delayed salaries

Palestinian teachers in the West Bank on Thursday began a strike demanding that the government pay their delayed salaries...

Libyans cast votes on mechanism to select top officials

The participants in the Libyan political dialogue forum started on Thursday to vote on the proposals and suggestions over...

Restaurants and gastropubs to reopen from tomorrow

Under the second stage of the easing of Level 5 restrictions, cafes, restaurants and bars serving food will be...

Hopes rising for speedy care home vaccination in the North

Hopes are rising that Northern Ireland could find a way of delivering vaccine more speedily to care homes. The size...

Minister: Bahrain to label settlement products as Israeli

An Israeli journalist wrote Thursday on Twitter that Bahrain's Industry, Commerce and Tourism Minister said his country "will NOT...

Must read

You might also likeRELATED
Recommended to you