Namungo watua Dar, wasubiri hatma ya CAF

-

Wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, klabu ya Namungo hatimaye imefanikiwa kurejea nchini salama ikitokea nchini Angola baada ya mchezo wake wa mtoano dhidi ya Premiero De Agosto kufutwa na CAF kutokana na kuhusishwa na Covid-19.

Wachezaji wa Namungo wakifanyiwa ukaguzi baada ya kutua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere jijini Dar es Salaam, Tanzania usiku wa jana.

Namungo iliondoka nchini Ijumaa tarehe 12 Februari 2021 kuelekea nchini Angola kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya klabu ya Premiero de Agosto ambao ulipangwa kuchezwa tarehe 14 Februari 2021.

Baada ya kuwasili nchini Angola na kufanyiwa vipimo, wachezaji watatu na kiongozi mmoja wa Namungo walikutwa na maambukizi ya Covid-19 na kulazimika kuanza matibabu haraka na msafara uliosalia ukaelekezwa kukaa karantini kwa muda wa siku tatu ama kurejea nchini Tanzania.

- Advertisement -

Klabu ya Namungo haikuafiki kukaa karantini kwa siku 3 kwa hisia kwamba huenda ni mbinu za kijanja janja za kuwatoa mchezoni.

Baada ya vuta nikuvute hiyo, Shirikisho la soka barani Afrika CAF, ikatangaza kuufuta mchezo huo siku ya Jumapili tarehe 14 Februari 2021 na kulipeleka suala hilo kwenye kamati yake ya maamuzi ili kutoa ufumbuzi wa sakata hilo.

Licha ya mchezo kufutwa na Namungo kulazimika kurejea nchini, lakini serikali ya Angola ikazuia wachezaji watatu na kiongozi mmoja wa klabu hiyo kurejea nchini kwasababu wanamaambukizi ya Covid-19 hivyo watawagharamia na kuwarejesha nchini wakipona ugonjwa huo.

Kocha wa klabu ya Namungo, Hemed Suleiman Morocco, amesema wanashukuru Mungu kwa kilichotokea kwani wamepata funzo kubwa kwenye michuano hiyo na kusisitiza kutozungumza mengi ya zaidi na kuwataka Watanzania wawaombee dua warejee salama nchini.

Sakata hilo likaishia kwa klabu ya Namungo kurejea nchini Tanzania na msafara wa wachezaji 19 na baadhi ya viongozi mishale ya saa 4 kasoro robo usiku wa jana Jumatatu ya tarehe 15 Februari 2021 huku wakisubiri maamuzi ya CAF juu ya hatma ya mchezo huo.

- Advertisement -
Publisher
Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

Latest news

Must read

You might also likeRELATED
Recommended to you