Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Lindi inaawashikilia Mkurugenzi wa kampuni ya Mafubilo inayojihusisha na uendeshaji maghala, Bakari Said na watendaji wa vyama vya ushirika kwa tuhuma za kula njama na kugushi stakabadhi ya malipo ya wakulima.
Akizungumza na waandishi wa habario leo Februari 22, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Lindi, Abnery Mganga amewataja Banaventure Mchemba (Ndomoni) na Conslata Msaki (Ukombozi) wa wilaya ya Nachingwea , ambapo amesema pia wameghushi na stakabadhi ya mazao ya tani 35 na kufanikiwa kulipwa zaidi Sh73.66 milioni.
Akieleza jinsi watuhumiwa hao walivyotenda makosa yao, Kamanda Mganga amesema mnamo Januari 29, Takukuru ilipokea taarifa ya njama na udanganyifu zilizofanywa katika ghala kuu la Pachani wilayani Nachingwea.
Katika taarifa hiyo, Kamanda Mganga amesema kampuni ya Mafubilo General Supplies ikishirikiana na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika Ndomoni na Ukombozi wanadaiwa kula njama na kugushi na kulipwa Sh73.66 milioni katika akaunti zao binafsi kinyume na sheria.
“Tunawashikilia viongozi wa vyama vya ushirika Ndomoni na Mkombozi vya wiliaya Nachingwea Bonaventure Mchemba , Conslata Msaki na Mkurugenzi wa Mafubilo General Supplies Ltd, Juma Bakari Saidi kwa tuhuma za utakatishaji fedha,” alisema Maganga
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo walifanya uchunguzi na kubaini kuwa, watuhumiwa baada ya kulipwa walihamisha fedha hizo kwenye akaunti ya Juma Bakari Saidi ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya Mafubilo.
Alisema vitendo hivyo ni makosa kwa mujibu wa Sheria ya kupambana na kuzuia Rushwa ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya utakatishaji fedha haramu AML ya mwaka 2012.
Aliongeza kuwa watuhumiwa walikiri kufanya udanganyifu huo na kuamua kurejesha fedha zote na kuzilipa kwenye akaunti ya Takukuru mkoa wa Lindi.