Watu wasiojulikana wamewapiga risasi na kuwauwa wanawake wanne wanaofanya kazi ya misaada kaskazini magharibi mwa Pakistan hivi leo.
Polisi wanasema wanawake hao waliokuwa wakifanya kazi na shirika moja lisilo la kiserikali wameuawa wakiwa kwenye gari yao katika jimbo la Waziristan, ambalo limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanamgambo wa siasa kali.
Hakuna kundi ambalo hadi sasa limebeba dhamana ya mauaji hayo, lakini mkuu wa polisi wa eneo hilo, Shafiullah Gandapur, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wana uhakika ni makundi aliyoyaita ya kigaidi.
Mnamo mwaka 2012, wanamgambo wa Taliban nchini Pakistan walimpiga risasi na kumjeruhi vibaya msichana Malala Yousufzai kwa kupigania elimu ya wasichana wenzake katika maeneo hayo hayo. Mwaka 2014, Malala alitangazwa kuwa mshindi wa kwanza mdogo kabisa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel.