By Charity James

KIRAKA mpya wa Yanga, Yanick Bangala anawapa mtihani mastaa tisa wanaoanza kikosi cha kwanza katika timu hiyo, kwani wakizubaa tu imekula kwao.

Bangala ni injini ndani ya kikosi hicho na watakaoepuka mtihani wake ni Kipa Djigui Diarra na mastraika Fiston Mayele na Heritier Makambo ambao hawezi kufanya majukumu yao.

Jamaa ni noma, anacheza nafasi saba kwa kiwango cha juu, ambapo mastaa wanaofanya majukumu hayo, mmojawao akipatwa na dharula kocha Nesreddine Nabi hawezi kupasua kichwa mbadala wake.

Uthibitisho wa kile alicholiambia Mwanaspoti, alicheza dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold akiziba nafasi ya Bakari Mwamnyeto aliyeumia katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba. Mechi yake ya kwanza dhidi ya Simba, Bangala alicheza kiungo mkabaji na aliwapa kazi ngumu mastraika wa Simba.

Mastaa ambao wana kazi ya kulinda viwango vyao mbele ya Bangala ni mabeki wa kati Dickosn Job na Mwamnyeto, Kibwana Shomari (beki 2), Mukoko Tonombe (kiungo 6), Zawadi Mauya (kiungo 8), Deus Kaseke na Dickson Ambundo, Farid Mussa (mawinga 7, 11) na Shaban Djuma (3).

Bangala aliliambia gazeti hili kuwa katika nafasi saba anazoweza kuzicheza hahitaji maandalizi hata kocha wake akimwambia siku ya mechi atamudu majukumu kama kawaida.

Advertisement

“Soka lipo kwenye damu, ilikuwa ndoto yangu kubwa. Ndio maana naweza kucheza nafasi hizo kwasababu ni kazi ninayoipa muda wangu mwingi. Najifunza na kufanya bidii, siridhiki na nilichofanya jana, natamani mapya kila ninapokuwa uwanjani,” alisema Bangala.

“Kocha akinianzisha muda wowote kwenye nafasi hizo nitamfanyia kazi yake vizuri. Nafasi ambazo zimenishinda ni straika na kipa, ingawa naweza kufunga vilevile.”

Yanga ilimsajili Bangala kutoka AS Vita ya DR Congo kwa mkataba wa miaka miwili na tayari alianza kuonyesha makali katika mechi tatu alizoanzishwa.

WASIKIE MAKOCHA

Mkurugenzi wa ufundi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Mirambo alisema wachezaji kama Bangala kwenye Ligi Kuu ni wachache wanaoweza kufanya vitu anavyovifanya kwa sababu anaweza kutimiza majukumu kwenye kila nafasi anayopangwa.

“Mchezaji amegawanyika katika maandalizi ya makundi mawili – kundi la kwanza ni hatua ya kuandaliwa na hatua ya ushindani ambayo inaanzia miaka minne hadi 12. Kwenye hatua hiyo mchezaji anakuwa hana nafasi maalumu ya kucheza na kwa maana hiyo sehemu ambayo kunakuwa na kocha mwenye uelewa anamfanya mchezaji acheze nafasi zote uwanjani,” alisema.

“Hayo yanatokea kwenye elimu aliyoipata kama kapita kwenye maandalizi ya mchezaji aliyepita kwenye shule za soka. Wachezaji wengi wanaokuja kuteka soka letu wanacheza nafasi moja kwa sababu wanamudu majukumu ya eneo hilo na hawawezi kufanya majukumu mazuri kwenye nafasi nyingine tofauti na Bangala ambaye nimemuona akicheza nafasi mbili tofauti na zote katimiza majukumu.”

Mirambo alisema unatakiwa kuwa ‘profesheno’ ili uweze kucheza nafasi nyingi uwanjani na kwa usahihi kwa sababu kila nafasi ina mahitaji yake, hivyo inatakiwa kutumia akili.

Naye kocha msaidizi wa Mwadui FC, Adolf Rishard alisema ni mchezaji muhimu ndani ya timu huku akiweka wazi kuwa kocha akiwa na wachezaji wawili kama hao kwenye timu anapunguza mahitaji ya wachezaji wengi.

“Ubora wa Bangala ni funzo kwa wachezaji wanaocheza eneo hilo, kwani kila akipewa nafasi ya kucheza anafanya kwa usahihi, hivyo ni wakati wa wachezaji wanaocheza nafasi hizo kujitafakari kwa kuongeza viwango ili wakipata nafasi wasitoe mwanya wa nyota huyo kupita nafasi zao,” alisena.

“Mukoko, Mwamnyeto wajitafakari, kazi sio ndogo kwao kwa sababu mchezaji huyo amefanya majukumu yao kwa usahihi na kupunguza makosa ya wachezaji hao ambayo walikuwa wakiyafanya walipokuwa wakipata nafasi.”

Rishad alisema ubora wa mchezaji anayecheza nafasi nyingi uwanjani ni bora kwa sababu anaweza kucheza vizuri kwa kujua nini afanye kwa wakati gani, na ni kutokana na uimara wake wa kucheza maeneo mengi anaweza kuhama eneo muda wowote.News Source link

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles