Bangala: Tumewasikia – Mwanaspoti

0
1

By Khatimu Naheka

KATIKA mechi tatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Geita Gold, Yanga imeshinda kwa bao 1-0 na kuwafanya mashabiki kukosa cha kuwatambia watani wao.

Lakini, beki na kiraka wa timu hiyo, Yannick Bangala amewaambia wamesikia kilio chao na kusisitiza kuanzia mechi zijazo watakata kiu yao na kufunga mabao mengi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bangala alisema hana wasiwasi na ubora wa safu ya ushambuliaji na kwamba mpaka sasa hakuna kibaya kinachofanyika na timu yao inashinda.

Bangala alisema baada ya ligi kurejea timu yao itakuja kushinda kwa mabao mengi ambapo washambuliaji wao watazidi kujuana na kucheza kwa utulivu.

“Sioni kama washambuliaji wana shida, tuna watu bora sana kule mbele, jambo la muhimu ni kuwapa muda, mashabiki wataona mabao mengi wakiendelea kuzoeana taratibu,” alisema Bangala ambaye ni mmoja wa mastaa waliorejesha ubora katika kikosi cha Yanga.

“Timu inashinda, ni kweli tunahitaji mabao zaidi ili kuwa na ushindi mzuri hicho ndio mashabiki wanataka na kwa timu ninavyoiona watafurahi tu ndani ya mechi zijazo.

Advertisement

“Kitu kizuri kwetu tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini pia yapo mabao yanafungwa, ila bahati mbaya waamuzi waliyakataa, hii kutengeneza nafasi tu ndio kitu muhimu ambacho kitaleta mabao mengi.”

Wasikie makocha

Akizungumzia suala la mabao Yanga, kocha wa zamani wa Yanga Princess, Edna Lema alisema: “Nafikiri Bangala yupo sahihi kwenye hilo, sioni kama Yanga iko vibaya, timu yao inashinda lakini kitu bora zaidi ni kama anavyosema Bangala kwamba wanatengeneza nafasi za kutosha na binafsi washambuliaji wanaotengeneza nafasi ndio watu bora kwenye timu.”

Lema pia ni kocha wa kikosi cha wanawake cha Taifa chini ya miaka 20.

Kocha Abdul Mingange alisema suala la mabao ndani ya Yanga ni jambo la muda tu na kwamba kama washambuliaji watakapoongeza utulivu wataanza kuvuna mabao mengi. “Bangala ni mchezaji mzoefu, kauli yake sina mashaka nayo, nilisema huko nyuma kwamba eneo kubwa ambalo liliiangusha Yanga msimu uliopita ni ubora wa washambuliaji na hivi sasa wameleta watu bora ambao wanajua kuamua mechi,” alisema Mingange.

“Hawa washambuliaji nawaona watafunga sana kwa sababu wanacheza sambamba na viungo bora, Yanga kushinda kwa mabao mengi ni suala la muda tu timu yao kama wataendelea kupata mafundisho ya kufunga kwa utulivu watashinda sana.”

Yaanzia gym

Jana, Yanga ilianza kazi rasmi ya mazoezi makali na baada ya kufuta safari ya kwenda jijini Arusha kwa ajili ya kambi fupi wameamua kujiandaa na mechi za Ligi Kuu wakiwa jijini Dar es Salaam na kuanzia gym.

Mabosi wa Yanga wameshtukia ratiba yao ya kambi wakiona ni kama watapoteza fedha na zaidi wakaamua kubaki palepale kambini Avic, huku jana wakianzia gym ili kuwapa stamina wachezaji wao kabla ya jioni kurudi uwanjani.

Yanga inajiandaa na mechi ya tatu ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC itakayopigwa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma Oktoba 19, baada ya we-nyeji wa mchezo huo, Vijana wa Kinondoni kuamua kuupeleka huko ikiwa ni mara ya pili kuisafirisha Yanga, kwani msimu uliopita walienda Jijini Mwanza.News Source link