By Saddam Sadick

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeyalimethibitisha kutokea mauaji ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa, Edward Ndonde anayedaiwa kuuawa kikatili kwa kuchomwa visu na mtoto wake, Mussa ambaye ni mtumishi wa Ruvu JKT.

Mussa anadaiwa kufanya mauaji hayo leo Jumatano Januari 12, 2022 nyumbani kwa baba yake mtaa wa Lumbira Kata ya Iwambi jijini Mbeya.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Christina Musyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa chanzo ni kutuhumiana kwa mambo ya kishirikina.

Amesema mtuhumiwa ambaye ni mtumishi wa Ruvu JKT, amekamatwa baada ya kutenda tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ili hatua za kisheria ziweze kushika mkondo wake.

“Ni kweli tukio lipo na limetokea leo, ambapo pia marehemu alikuwa mwalimu msitaafu, chanzo kinadaiwa kuwa mambo ya kishirikina, ambapo mtuhumiwa alikuwa anamtuhumu baba yake kuwa ni mchawi na Jeshi la Polisi limemshikiria kwa uchunguzi zaidi” amesema Christina.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Alhaji Saad Kusilawe amesema marehemu aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa ambapo aliitumikia kwa muda wote na kwa uadirifu na kwamba wanasubiri maelekezo kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Advertisement

“Tumepoteza hazina ya kiongozi, kwani katika utumishi wake aliweza kumaliza vyema hadi anastaafu, ni pigo kubwa na ni masikitiko makubwa” amesema Kusilawe.

Naye Balozi wa Mtaa huo, Hezron Thobias amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alianza kutamka maneno kuwa amemaliza kazi yake aliyoitiwa na baba yake ya kuchinja kuku, jambo lililowashtua na kwenda kuangalia waliposikia kelele zikitoka ndani.

“Alionekana kama ana ugoro na amelewa, akawa anatamka maneno kuwa amemaliza kuchinja kuku, tukamuona Mama yake analia anasema njoo muone mtoto alichofanya akiwa anatokwa machoji, ile tunaingia ndani tukakuta amemuua damu zimemwagika” amesema Thobias.

Mwananchi imefika nyumbani kwa marehemu huyo na kukuta vilio na simanzi vikitawala huku majirani na waombolezaji wakiendelea na taratibu msiba.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles