By Stephano Simbeye

Songwe: Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa kimelaani tukio la ofisi yao katika Jimbo la Tunduma mkoani Songwe, kuchomwa moto na watu wasiojulikana.

Tamko hilo limetolewa leo Jumatano Oktoba 13, 2021 na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa aliyesema huo umekuwa mwendelezo wa ofisi zao kuchomwa moto katika baadhi ya maeneo nchini.

Mchungaji Msigwa ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuchukua hatua ikiwemo kuchunguza masuala yanayohusu chama hicho.

“Ikumbukwe miezi michache hapo nyuma vizimba vyetu pale Tunduma vilivunjwa na mpaka sasa Polisi hawajachukua hatua na kuwakamata waliohusika,” amesema Msigwa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba, uchunguzi ikiwemo kuwabaini watu waliohusika unaendelea.

Amesema kuwa Polisi wamebaini kuwa katika tukio hilo nyaraka ndio zimechomwa na kwamba, jengo halikuunguzwa.

Advertisement

“Mlango wa ofisi umevunjwa kisha nyaraka kuchomwa moto zikiwemo baadhi ya nguo. Lakini ndani ya ofisi kulikuwa na meza na viti amnavyo havikuungua. Bado tunaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika na tukio hilo,” amesema Kamanda Magomi.

Awali, Katibu wa Chadema Jimbo la Tunduma, Osia Kibwana amesema vitu vilivyochomwa ni pamoja na vitabu, bendera za chama, mihuri na hati mbalinbali za umiliki wa mali za chama vikiwemo za viwanja.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles