By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Dawa inayotibu virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Uviko-19, zimeanza kufanyiwa majaribio mapema wiki hii kwa watu 2,660 ikiwa ni miezi 13 tangu kupatikana kwa chanjo.

Kufuatia ujio wa dawa hiyo, watafiti mbalimbali nchini na duniani wamesema kuwa iwapo dawa hiyo itafaulu, dunia itapata tiba na kutakuwa na uwezekano mkubwa ikadhibiti virusi vya corona kabla havijaenea zaidi na kuwa mbadala wa chanjo.

Dawa hizo za kumeza zilizotengenezwa na Kampuni ya kutengeneza dawa nchini Marekani ya Pfizer, watapatiwa wale wanaoishi na mtu aliyeambukizwa ambayo pia imelenga kuwazuia wale ambao hawana dalili zozote za maambukizi dhidi ya kupata virusi hivyo.

Mkuu wa Utafiti wa kisayansi kwenye kampuni hiyo, Dk Mikael Dolsten alisema dawa hiyo itafanyiwa majaribio kwa watu 2,660 wenye umri wa kuanzia miaka 18 wenye afya njema na wanaoishi nyumba moja na mtu aiyewahi na aliyepata maambukizi ya ugonjwa huo.

“Pfizer pia tunafanya majaribio ya dawa hii kwa watu ambao tayari walipata corona ingawa hawajaonyesha dalili zozote za maambukizi,” amesema Dk Dolsten.

Hata hivyo wataalamu wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji na wafamasia nchini wanasema iwapo majaribio ya dawa hiyo yatafanikiwa, utakua ni mwanzo mzuri wa tiba ya ugonjwa huo pia.

Advertisement

Mfamasia na Mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba amesema ujio wa dawa hiyo utasaidia kwa kuwa dunia ilijielekeza kwneye kukinga pekee.

“Upo uwezekano mkubwa dawa hii ikasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya huu ugonjwa, changamoto ni kubadilika kwa kirusi, tusubiri majibu ya utafiti. Hili si suala jipya ni suala ambalo linawezekana kwa teknolojia tuliyonayo hivi sasa,” amesema Myemba.

Amesema ijapokuwa tunazo chanjo kwa ajili ya kupata kinga wapo wanaopata ugonjwa mkali hivyo kama ikipatikana dawa itakua msaada, “Kama kuna dawa inayotibu itasaidia zaidi hivyo chanjo na dawa zikitumika kwa pamoja tutapata matokeo chanya.”

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji na magonwja ya ndani, Elisha Osati amesema, “Inategemea na matokeo ya utafiti. Kama itaonyesha inasaidia, itakuwa jambo zuri sana na kuwa mbadala wa chanjo.”

Mtendaji mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la RBA Initiative ambaye pia ni Mfamasia, Erick Venant amesema huo ni mwendelezo wa juhudi za wanasayansi ulimwenguni kote katika kutafuta tiba ya Uviko-19.

“Tayari tuna chanjo kadhaa  lakini kuanza kwa majaribio (clinical trials) kwa dawa ambayo itaweza kudhibiti virusi vya corona baada ya mtu kuwa tayari kapata ugonjwa huo ni hatua muhimu katika kupambana na Uviko-19.

“Dawa hii pia itasaidia kuzuia madhara makubwa, kama majaribio hayo yatafanikiwa itakuwa hatua nzuri katika kudhibiti huu ugonjwa.

“Hatahivyo ni vyema watu kuendelea kufuata hatua zote za kujikinga na Uviko-19 na maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya wakati huu ambapo juhudi mbalimbali za kudhibiti ugonjwa huu zinaendelea,” amesema Venant.

Ametoa rai kwa jamii kujiepusha na matumizi holela ya dawa za antibiotiki bila kupima na wala kuwa na cheti cha daktari.

“Kipindi hiki cha Uviko-19 pia matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanaongezeka. Hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kitaalamu (Antimicrobial resistance) ni vyema kutumia dawa mara tu baada ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya,” amesema.

Katika hatua nyingine shirika la Reuters leo Septemba 30 limeripoti kuwa kampuni hiyo kwa kushirikiana na BioNTech inatarajia kuanza kutoa chanjo ya Uviko-19 kwa watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 11.

Mmoja wa watafiti Dk Anthony Fauci amesema ikiwa uamuzi wa Shirika la Chakula na madawa (FDA) utaidhinisha chanjo hiyo  iliyotengenezwa na Pfizer / BioNTech itaanza kutolewa kwa watoto ifikapo Novemba mwaka huu.

Mpaka mchana wa leo, idadi ya walioambukizwa virusi hivyo duniani kote ni zaidi ya milioni 234.1 huku  zaidi ya milioni 4.8 waliripotiwa kufariki kwa mujibu wa wavuti wa Covid-19 wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles