Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmshauri kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo Oktoba 6, 2021 amefanya ziara ya Chama Mkoa wa Pwani ili kufuatilia maendeleo ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na Maendeleo ya Mkoa kwa ujumla.

Dkt. Mpango amewapongeza na kuwashukuru viongozi na wananchi wa Mkoa wa Pwani kwa kuendelea kudumisha Amani na Usalama wa mkoa  huo. Amesema ili kupata maendeleo ya haraka katika mkoa huo, wananchi hawana budi kuendelea kuitunza Amani iliopo.

Aidha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewapongeza wanachama na viongozi wa CCM mkoa wa Pwani kwa kuendelea kujiimarisha kiuchumi ikiwa ni pamoja kuanzisha miradi inayosaidia katika uendeshaji wa chama hicho mkoani Pwani.  Ameeleza kwamba siasa safi zinaendana na uchumi imara hivyo amewasihi kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kufanya uwekezaji wenye tija. Amesema ni muhimu kuendelea kugharamia uchaguzi kwa fedha za chama ili kuepuka kupata viongozi wenye maslahi binafsi katika uongozi wao.

Amewasihi wananchama wote wa CCM Pwani kujiepusha na migogoro na makundi ndani ya chama pamoja na kuwaagiza kuongeza ushirikiano baina ya chama na serikali.

Aidha ameeleza ni muhimu kuendelea kuwajengea uwezo wanachama na viongozi kupitia semina na mafunzo mbalimbali ili kuweza kuendana na ushindani wa kisiasa. Amewaagiza viongozi na wanachama kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020 pamoja na kuisimamia serikali ili kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka.

Amewataka viongozi wa CCM Pwani kuendelea kuongeza wanachama na kuhimiza ulipaji wa ada za uanachama ili kuwezesha chama kujiendesha bila utegemezi. Amesema ni muhimu kwa wanachama kujiunga na kadi za uanachama za kielekroniki pamoja na kuanza mikakati ya mapema ya uchaguzi ndani ya chama unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameagiza wabunge wanaotokana na CCM mkoa wa Pwani kuhakikisha wanafanya ziara ili kupokea kero za wananchi waliowachagua na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kutoa taarifa kwa wananchi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea hapa nchini.

Makamu wa Rais ametumia mkutano huo kusisitiza madawati ya utoaji huduma za afya kwa wazee katika vituo vya kutolea huduma za afya yanatakiwa kufanya kazi kadri ya miongozo na taratibu zilizowekwa ili kuondoa changamoto zinazowakabili wazee katika maeneo ya huduma za afya.

Aidha amewasihi wananchi wa Pwani kuendelea kujilinda na Uviko 19 pamoja na kuhamasisha wananchi wengi Zaidi kupata chanjo ya ugonjwa huo. Amesema serikali imewaletea chanjo hiyo salama wananchi katika maeneo yote nchini hivyo hawana budi kujitokeza kwa wingi ili kuendelea kupunguza madhara ya ugonjwa huo.