By William Shao

Tangu alipoiondoa madarakani serikali ya Mfalme Idris, Muammar Gaddafi alikaa madarakani kwa miaka 42 hadi naye alipoondolewa madarakani kwa njia zile zile ambazo yeye alizitumia kuiangusha serikali ya Idris.

Kutokana na wimbi la maandamano lililozikumba baadhi ya nchi za Kiarabu mwaka 2011, Gaddafi alimtetea Rais wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali, ambaye wakati huo alikuwa anakabiliwa na mapinduzi.

Mapinduzi ya Tunisia, ambayo pia huitwa Mapinduzi ya Jasmine, yalikuwa kampeni kubwa ya siku 28 ya raia wa nchi hiyo kuipinga serikali yao iliyoongozwa na Ben Ali.

Maandamano hayo yalijumuisha mfululizo wa maandamano ya barabarani nchini Tunisia, na kusababisha kuangushwa kwa Rais Ben Ali Januari 14, 2011 ambaye alikuwa amekalia kiti hicho kwa miaka 24 tangu Novemba 7, 1987.

Wakati wa maandamano ya Tunisia, Gaddafi alisema kwamba watu wa Tunisia wataridhika ikiwa Ben Ali angeanzisha mfumo wa Jamahiriyah. Huo mfumo uliasisiwa na Gaddafi mwenyewe mwaka 1977 ukimaanisha ‘Taifa la Umma’ yaani raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia ‘kamati za umma’.

Awaita maadui zake waasi

Advertisement

Kwa kuogopa maandamano ya ndani, serikali ya Libya ilitekeleza hatua za kuzuia kwa kupunguza bei za chakula, kuwaondoa kwenye uongozi maofisa wa jeshi waliodhaniwa kuwa ni waasi na kuwaachilia wafungwa kadhaa wa Kiislamu.

Lakini hatua hizi na nyingine alizochukua hazikufanikisha alichokusudia, kwa sababu alichohofia kilijitokeza Februari 17, 2011, wakati maandamano makubwa yalipozuka dhidi ya serikali yake.

Tofauti na ilivyokuwa Tunisia au Misri, kwa sababu ya kufuata sana dini, Libya haikuwa na harakati kali za Kiisilamu, lakini kwa sehemu kubwa raia wa nchi hiyo hawakuridhishwa na utawala wa Gaddafi kwa madai kwamba ulianza kukumbatia ufisadi na kuvumilia ufisadi na mifumo iliyojaa ya upendeleo, huku ukosefu wa ajira ukiwa umeongezeka na kufikia karibu asilimia 30.

Gaddafi aliwashutumu waandamanaji hao na kuwaita ni waasi “waliolishwa dawa za kulevya” na akawahusisha na kundi la ugaidi la al-Qaeda. Kisha akasema atakufa akiipigania Libya kuliko kuikimbia nchi hiyo.

Alipotangaza kwamba waasi hao “watawindwa mitaani, barabara, nyumba kwa nyumba na hata kabati kwa kabati,” jeshi liliwafyatulia risasi waandamanaji huko Benghazi, na kuua mamia miongoni mwao.

Wakishtushwa na kitendo cha serikali, wanasiasa kadhaa waandamizi walijiuzulu au walijiunga na upande wa waandamanaji. Uasi huo ulienea haraka upande wa mashariki mwa nchi hiyo ambayo haikuwa imeendelea kiuchumi nchini Libya.

Kwa kushtushwa na mambo yaliyokuwa yakiendelea nchini Libya ya waandamanaji kuuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa nchi hiyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilishutumu vikali matumizi ya nguvu dhidi ya raia nchini humo, na kutoa wito kwa wale wanaohusika katika uovu huo dhidi ya raia kuwajibikia kwa makosa yao.

Soma zaidi:Gaddafi mtata tangu utotoni

Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo ya dharura jijini New York, Marekani, ilitaka kukomeshwa kwa vurugu mara moja na kutoa wito kwa maofisa kushugulikia malalamiko ya wananchi wa Libya.

Lakini baraza hilo halikushughulikia ombi la naibu balozi wa Libya katika Umoja wa Mataifa, Ibrahim Dabbash, la kutaka anga zote za Libya kufungwa ili kuzuia mashambulio dhidi ya waandamanaji. Dabbash alisema wanajeshi wa serikali wameanza kuwashambulia raia magharibi mwa Libya.

Awali Waziri wa usalama wa ndani wa Libya, Abdel Fatah Yunes, alijiunga na orodha iliyoongezeka ya maofisa waandamizi katika serikali ya Gaddafi waliojiuzulu. Alilitaka jeshi la taifa hilo kujiunga katika mapinduzi ya kumng’oa madarakani Kanali Gaddafi.

Soma zaidi: Gaddafi aandaa vikosi vya siri akiwa shuleni

Spika wa Bunge la Libya alitoa tangazo kwenye televisheni ya taifa kuhusu kile alichokitaja kama uchunguzi huru kuhusu matukio yaliyotokea. Alisema serikali inabuni utitiri wa sheria mpya, ikiwamo sheria za vyombo vya habari na katiba ya kudumu.

Aaapa kufia Libya

Jumanne ya Februari 22, mwaka huo ikiwa ni miezi minane kabla ya kukamatwa na kuuawa, Kanali Gaddafi alilihutubia taifa. Katika hotuba hiyo kubwa zaidi tangu maandamano kuanza wiki moja iliyokuwa imepita, Kanali Gaddafi alisema kuwa yuko tayari kufa nchini mwake iwapo italazimika. Akizungumza nje ya mahali aliposema kuwa ni makao yake mjini Tripoli, Gaddafi alitoa wito kwa wafuasi wake kujitokeza mitaani kuvunja maandamano dhidi ya serikali.

Katika hotuba yake Gaddafi alisema kutokana na utawala wake, Libya imekuwa taifa linaloongoza duniani. Alikaririwa akisema: ‘’Mimi ni mpiganaji, mimi ni mpiganaji kutoka vijijini, kutoka jangwani. Nimepigana mijini na vijijini katika mapinduzi ya kihistoria yaliyoleta heshima kwa nchi ya Libya. Watajivunia mafanikio yake kizazi baada ya kizazi.”

Aliendelea kusema: ‘’Babu yangu Abdulsalam Bu-Munyar ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kujitoa mhanga wakati wa vita. Kwa hiyo siwezi nikavunja mwiko huo. Sitaondoka kwenye ardhi hii ya nchi yangu yenye heshima. Nitajitolea mhanga kupigania nchi yangu hadi mwisho.”

Kisha akaonya kuwa mtu yeyote atakayeshiriki katika maandamano hayo atahukumiwa kifo. Aliwaita waandamanaji ha kuwa ni “mende” au “panya”.

Hali mbaya kwa Gaddafi

Hali ilizidi kuwa mbaya kwa miezi michache iliyofuata kiasi kwamba maandamano yalisogea hadi karibu na makazi ya Gaddafi baada ya waasi kudhibiti sehemu kubwa ya mji wa Tripoli Jumapili ya Agosti 21, 2001.

Usiku wote wa kuamkia siku hiyo kulikuwa na umati wa watu wakishangilia katika bustani ya Green Square, awali eneo hilo lilikuwa likiwakilisha sura ya maandamano ya watu wanaomuunga mkono Gaddafi. Waasi walikumbana na upinzani mdogo walipoingia kutokea mashariki, kusini na magharibi.

Kufikia tarehe hiyo, msemaji wa waasi alisema majeshi ya Gaddafi bado yanadhibiti asilimia 15-20% ya Tripoli na kwamba tayari walikuwa wamemkamata mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi, Saif al-Islam.

Kufikia hatua hii, ilionekana dhahiri kwamba mwisho wa Gaddafi ulikuwa umefika na waasi wamefanikiwa kupata kile walichokuwa wakikitaka. Katika bustani ya Green Square, raia waliounga mkono waasi walichana bendera za kijani za serikali ya Gaddafi na kukanyaga picha zake.

Rais wa Marekani, Barrack Obama, alikaririwa akisema: “Wakati wa kuupinga utawala wa Gaddafi sasa umefikia kilele chake. Tripoli inaanguka kutoka mikononi mwa dikteta.”

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye alisitisha likizo yake kusimamia kikao cha Baraza la Usalama la Taifa alisema ni wazi: “Sasa mwisho wa Gaddafi umekaribia … (Gaddafi) amefanya uhalifu dhidi ya watu wa Libya na lazima aondoke sasa kuepusha mateso zaidi kwa watu wake”.

Huo ndio ule wakati ambao Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa mjini The Hague ilikuwa katika majadiliano ya kumhamisha mtoto wa Gaddafi, Saif al-Gaddafi, kwenda kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita. Mahakama hiyo pia ilikuwa inatafuta kumkamata Kanali Gaddafi na mkuu wake wa Usalama, Abdullah al-Sanussi.

Wakati huo huo mtoto mwingine wa Gaddafi aliyeitwa Muhammad, alizungumza kwa simu kupitia Televisheni ya al-Jazeera wakati waasi walipoizunguka nyumba yake. Milio ya risasi ilisikika kabla ya mawasiliano kukatika.

Tangu Mei mwaka huo Kanali Gaddafi hakuwa ameonekana hadharani, ingawa alikuwa akitoa matangazo ya redio kutoka maeneo yasiyojulikana.

Agosti 22 uongozi wa waasi, Baraza la Mpito la Taifa (NTC), ukatangaza kuwa unahamisha makao yake makuu ya harakati kwenda Tripoli kutoka mashariki mwa mji wa Benghazi, ambao umekuwa mikononi mwa waasi tangu siku za mwanzo ya machafuko ya kisiasa.

Je, nini kilimfika Gaddafi hadi kufa kwake? Tukutane kesho ikiwa ni sehemu ya mwisho ya makala haya.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles