By Florah Temba

Moshi. Mkoa wa Kilimanjaro umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa nchini inayoendeleza mila kandamizi ikiwemo mfumo dume na kuwanyima wanawake fursa ya kumiliki ardhi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani humo, Edward Mpogolo leo Oktoba 14, 2021 wakati akipokea msafara wa kijinsia kuelekea Siku ya Mwanamke wa Kijijini  uliotokea mkoani Mwanza hadi Kilimanjaro, kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umiliki wa ardhi.

“Licha ya mwanamke kuwa kiungo kikubwa cha malezi ya familia, lakini inapokuja suala la umiliki wa ardhi unakuta wanaume ndiyo wanakuwa mbele na wanawake wananyimwa hiyo haki.

“Hata baadhi ya mila zetu, zinasema mwanamke haruhusiwi kumiliki ardhi na ikitokea baba amefariki, watu wengine wanarithi ardhi,” amesema DC Mpogolo.

Naye kiongozi wa msafara huo, ambaye ni Ofisa maendeleo ya Jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Janeth Shishila amesema msafara huo umepita umeelimisha jamii umuhimu wa mwanamke kumiliki ardhi kila ulikopita.

“Katika maeneo ambayo tumepita tumetoa elimu ya umuhimu wa mwanamke wa kijijini kumiliki ardhi kwa maendeleo ya familia.

Advertisement

“Tumebaini katika Mikoa mingi nchini, mila kandamizi ukiwemo mfumo dume, umekuwa kichocheo kikubwa cha kuwanyima wanawake fursa ya umiliki wa ardhi, maeneo mengine hawaruhusiwi kumiliki chochote katika familia na migogoro mikubwa ya ardhi inayotokana na wanawake kunyimwa kumiliki ardhi,” amesema Janeth.

Kwa upande wake, Mwanasheria kutoka Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (Tawla), Fatuma Kimwaga amesema uwepo wa mfumo dume ni moja ya changamoto inayowanyima wanawake, fursa ya kumiliki ardhi.

Siku ya mwanamke wa kijijini, ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 15, mwaka huu inaadhimishiwa mkoani Kilimanjaro, ikibebwa na kauli mbiu ya ‘Ardhi ni nyenzo ya maendeleo kwa mwanamke wa Kijijini.’

Maadhimisho hayo yameandaliwa na Serikali kwa kushirikuana na Tawla, Shirika la Kimataifa la Ardhi (Landesa) na mashirika yanayounda kikosi kazi cha kampeni ya Linda Ardhi ya Mwanamke (S4HL), We Effect, Tala na PWC.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles