By Florah Temba

Moshi. Kata tatu katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, zimewekwa  karantini ya mifugo, ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Kimeta, ambao viashiria vya ugonjwa huo vimeanzia katika Kata ya Mamsera wilayani humo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga, wakati akizungunza na gazeti la mwananchi, leo Oktoba 22, 2021, na kuzitaja kata hizo kuwa ni  Mamsera, Mahida na Chala na kwamba zitakuwa kwenye karantini hadi viashiria vya ugonjwa wa Kimeta vitakapoisha.

Mpaka sasa Watu wawili wanadaiwa kufariki dunia, baada yakula nyama ya ng’ombe inayodaiwa kuwa na ugonjwa wa kimeta, huku wengine zaidi ya 30, wakiathirika baada ya kula nyama hiyo na wengine wakilazwa hospitali kwa matibabu na wengine kupatiwa matibabu na kuruhusiwa.

Kanali Maiga amesema mpaka sasa mtu mmoja bado amelazwa Hospitali ya Ngoyoni akiendelea na matibabu, na kwamba watu wengine ambao walikula nyama hiyo, wameendelea kuchukua tahadhari ya kuhudhuria hospitali kupimwa ili kuona kama watakuwa na dalili za ugonjwa huo.

“Hatua mbalimbali zimechukuliwa baada ya kuonekana viashiria vya ugonjwa wa Kimeta na mojawapo ni kuziweka karantini kata tatu za Mamsera, Mahida na Chala.Hairuhusiwi mifugo kuingia wala kutoka katika kata hizi mpaka viashiria vya ugonjwa huu vitakapoisha,”amesema.

Jana Oktoba 21, 2021, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, alitoa taarifa ya uwepo wa dalili za ugonjwa wa Kimeta wilayani Rombo na kusema Watu wawili wamefariki dunia na mtu mmoja aliyepima Ng’ombe huyo na kuthibitisha yupo salama, amelazwa hospitali akiendekea na matibabu, huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Advertisement

“Oktoba 6, 2021, eneo la Mamsera, nyumbani kwa mwananchi mmoja, kulikuwa na Ng’ombe watatu na mmoja alikufa, mtu moja alijitokeza kuwa ni Mtaalamu wa mifugo akathibitisha Ng’ombe yule alikuwa mzima hana matatizo akagonga na mihuri ambayo nafikiri ilikuwa feki,”alisema mkuu wa mkoa.

Aidha alisema kuna uwezekano wa kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta, na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kuepuka kula nyama za mizoga kutokana na hofu ya ugonjwa huo wa Kimeta.

“Nitoe tahadhari kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro hususani Wilaya ya Rombo, kujiepusha kula nyama ya mizoga, kutokana ba tukio hili, lakini serikali bado tunaendelea na uchunguzi, ili kujua kama ni Kimeta au vinginevyo”

Mkuu huyo wa Mkoa, alitumia pia nafasi hiyo, kuwataka wananchi na wale wote wenye mabucha ya nyama mkoani humo, kuhakikisha nyama hizo zimepimwa na mtaalamu wa mifugo aliyethibitishwa.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles