By Emmanuel Mtengwa

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Januari 10, 2022 anawaapisha viongozi mbalimbali aliowateua juzi Jumamosi.

Wanaoapishwa leo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ni pamoja na mawaziri na naibu mawaziri wapya, makatibu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali walioteuliwa Jumamosi Januari 8, 2022.

Katika uteuzi huo uliofanya na Rais Samia na kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga juzi Jumamosi Ikulu jijini Dar es Salaam, Balozi Kattanga alitangaza mawaziri wapya watano na naibu mawaziri watano.

SOMA:Mawaziri wapya hawa hapa

Mawaziri hao wapya walioteuliwa ni; Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Hamad Masauni (Mambo ya Ndani), Dk Pindi Chana (Sera Bunge na Uratibu), Anjelina Mabula (Ardhi) na Hussein Bashe (Kilimo).

Naibu mawaziri wapya walioteuliwa ni; Anthony Mavunde (Kilimo), Jumanne Sagini (Mambo ya Ndani) DkLemomo Kiruswa (Madini), Ridhiwani Kikwete (Ardhi) na Atupele Mwakibete (Ujenzi na Uchukuzi).

Advertisement

Katika mabadiliko hayo madogo ya Baraza la Mawaziri, Mkuu huyo wa nchi aliwabadilisha na kuwahamisha mawaziri katika wizara tisa.

Mawaziri hao waliohamishwa wizara za awali ni wafuatao na wizara wanazohamishiwa katika mabano; Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ummy Mwalimu (Afya), George Simbachawene (Katiba na Sheria), Profesa Joyce Ndalichako (Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Innocent Bashungwa (Tamisemi).

Mawaziri wengine waliohamishwa ni; Profesa Adolf Mkenda (Elimu), Dk Doroth Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu), Mohamed Mchengerwa (Utamaduni, Sanaa na Michezo), Dk Ashatu Kijaji (Uwekezaji, Viwanda na Biashara).

Naibu mawaziri waliohamishiwa wizara ni pamoja na; Khamis Khamis (Muungano na Mazingira), Hamad Chande (Fedha na Mipango) na Mwanaidi Khamis (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu).

Katika mabadiliko hayo madogo ya Baraza la Mawaziri wapo waliokuwa mawaziri na naibu waziri ambao hawakuchaguliwa akiwamo aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji Geoffrey Mwambe, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbona aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mwita Waitara.

Rais Samia pia alifanya mabadiliko ya wizara tatu na kuunda wizara mpya ikiwamo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Wizara ya Afya na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Akitangaza mabadiliko hayo, Balozi Kattanga alisema Rais Samia ameteua makatibu wakuu wapya saba, naibu makatibu wakuu wapya wawili na kuhamisha makatibu wakuu sita huku huku wengine wakiachwa.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles