By Shaban Njia

Kahama. Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani mkoani Shinyanga limekamata mabasi matano kati ya 30 na kuyazuia kusafirisha abiria  baada ya kukutwa  na makosa mbalimbali.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba mosi, 2021 Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Shinyanga,  Malege Kilakala amesema pamoja na kukagua mabasi hayo pia wanatoa elimu  kwa abiria kuhusu usalama wao wanapokuwa safarini.

Amesema wamekagua mabasi yote yanayokwenda mikoani na kubaini 30 yana makosa mbalimbali na kuyatoza faini na kuendelea na safari lakini mabasi matano yalizuiwa kuendelea na  safari baada ya kukutwa na makosa kadhaa yakiwemo tairi kuisha na breki kutofanya kazi.

“Tumebaini magari mengi ni mabovu na yanahitaji kufanyiwa marekebisho madogomadogo, magari yaliyokuwa na matatizo ya kawaida tumeyapiga faini na kuyaacha yaendelee  na safari na yale mabovu zaidi tumesitisha safari,” amesema Kilakala.

Amewataka wamiliki wa mabasi hayo kuhakikisha  yanakuwa na ubora unaotakiwa  kabla ya  kubeba abiria kwa kuangalia mifumo ya taa, bodi pamoja na injini.

Mmoja wa abiria, Elizabetha Josephat amesema ukaguzi huo ni muhimu  kwani hakuna abiria ambaye hapendi kufika salama mahali  anapokwenda.

Advertisement

This article Belongs to

News Source link