By James Magai

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imeridhia maombi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kufungua rasmi shauri la kupinga tozo za miamala ya simu.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano, Oktoba 13, 2021 na Jaji John Mgetta, baada ya kukubaliana na maombi ya Asasi hiyo isiyo ya Kiserikali ya kibali cha kufungua shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama (Judicial Review) Sheria ya Mfumo wa Malipo na Kanuni zake, ambazo zimeanzisha tozo hizo.

Akitoa uamuzi huo Jaji Mgetta amesema kuwa, LHRC imekidhi vigezo muhimu vitatu vya kupewa kibali cha kufungua shauri hilo.

Akivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na kufungua maombi ya kibali hicho ndani ya muda wa miezi sita tangu kutangazwa kwa sheria husika.

Soma zaidi:Serikali ya Tanzania yaipinga kesi ya miamala ya simu

Jaji Mgetta amesema sheria hiyo ilitangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba Juni 30, 2021 na LHRC ilifungua shauri hilo Julai 27 mwaka 2021 na kwamba maombi hayo yaliwasilishwa ndani ya muda.

Advertisement

Kigezo cha pili Jaji Mgetta amesema kuwa ni mwombaji kuwa na hoja za msingi ambazo anataka zizungumzwe katika maombi yake na kwamba LHRC katika kiapo na maelezo yanayounga mkono maombi hayo kimethibitisha  kuna hoja za msingi. 

Soma zaidi:Kesi kupinga tozo miamala ya simu yaunguruma

“Hivyo ninaona kuwa mleta maombi (LHRC) ana madai ya msingi ambayo anapaswa kupewa nafasi kueleza ni kwa namna gani kuna tatizo katika sheria hiyo. Kwa hiyo kwa kutazama maombi yao ninaona kuwa kuna hoja ambazo mahakama inapaswa kuziangalia,” amesema Jaji Mgetta. 

Katika kigezo cha tatu Jaji Mgetta amesema kuwa mwombaji anapaswa kuwa na maslahi katika shauri husika na kwamba mwombaji katika kiapo chake ameeleza kuwa anamiliki simu na line za mtandao wa Tigo, Airtel na Vodacom ambazo anazitumia kutuma na kupokea fedha na kwamba hivyo ameathirika na sheria hiyo.

Soma zaidi: Maumivu ya tozo miamala ya simu

“Hivyo ninaona kuwa mleta maombi ana hoja na anapaswa asikilizwe. Kwa hiyo mleta maombi (LHRC) ameweza kukidhi vigezo vitatu hivyo ameruhusiwa kuleta maombi yake mahakamani,” amesema Jaji Mgetta akihitimisha uamuzi wake huo.

Awali LHRC kilitungua maombi hayo Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

LHRC katika shauri namba 11 la mwaka 2021, ilikuwa inaomba   kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama Kuu (Judicial Review) kuhusu Sheria ya Mfumo wa Malipo ya Sura 437 na Kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwenye simu.

Pamoja na mambo mengine ilikuwa ikidai kuwa tozo hizo zimekuwa ni mzigo mkubwa kwa wananchi.

Kabla ya usikilizwaji wa maombi hayo Serikali iliweka pingamizi la awali ikiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo kwa madai kuwa yana kasoro za kisheria huku ikibainisha sababu tatu.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles