Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo Septemba 30, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA).

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ametaja Michezo kama njia ya kuleta umoja na undugu katika maeneo ya kazi pamoja na kuondokana na maradhi mbalimbali. Amesema kupitia michezo ndio kunaweza pia kukabiliana na Uviko 19 pamoja na kutoa elimu ya kupata chanjo ya ugonjwa huo.  

Makamu wa Rais ametoa rai kwa Shimmuta kutumia michezo wanayoisimamia kutoa elimu ya utunzaji mazingira. Amesema yapo maeneo mengi yanayohotaji upandaji miti pamoja na usafi wa mazingira hivyo Shimmuta inapaswa kuwa chachu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa vitendo.

Aidha Makamu wa Rais ameiasa SHIMMUTA kufanya michezo itakayotoa mchango katika jamii kama vile Riadha zinazofanywa kwa lengo la kupata fedha na kusaidia katika  huduma za kijamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shimmuta, Hamis Mkanachi amesema changamoto inayoikabili Shimmuta ni ukosefu wa udhamini katika mashindano yanayoandaliwa pamoja ushiriki mdogo wa Mashirika, Kampuni na taasisi katika michezo hiyo.

Mashindano ya Shimmuta mwaka 2021 yanatarajiwa kufanyika mkoani Morogoro katikati ya mwezi Novemba.

 

Tagged in:

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles