Kituo cha kudhibiti magonjwa nchini Marekani (CDC) kimetoa tahadhari kwa raia wake kutofanya safari nchini Kenya kwa maelezo kuwa nchi hiyo ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya Covid-19, kitaalamu (A Level 4 alert).
Tahadhari hiyo imetolewa Aprili 07, ikionya juu ya usalama wa kiafya kutokana na kasi ya maambukizi ya corona nchini Kenya pamoja na ongezeko la uhalifu, ugaidi na utekaji.
Wasafiri wa Marekani wameshauriwa na CDC , kuangalia kurasa ya idara ya usafiri kabla ya kupanga safari yeyote kutokana na changamoto ya COvid 19.
Licha ya tahadhari hiyo kutolewa ndege za kimataifa bado zinafanya kazi nchini Kenya.
Mwishoni mwa mwezi Machi, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza zuio la kukutoka nje katika kaunti tano nchini humo ukiwemo mji mkuu Nairobi ,Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru ili kuzuia usambaaji wa virusi vya Corona .
Hatua hii ilikuja kwasababu Kiwango cha maambukizi kimezidi mara kumi zaidi kwa mujibu wa maelezo ya rais Kenyatta.
Hakuna usafiri wa barabarani ,angani na reli utakaoruhusiwa kuingia na kutoka sehemu hizo zilizotajwa kama zenye janga ‘zilizoathiriwa sana na Corona.