By Jesse Mikofu

Unguja. Moto umeteketeza maabara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Sayansi za Bahari na Kituo cha Taifa cha Takwimu za Bahari Tanzania mjini Unguja Zanzibar leo.

Hata hivyo licha ya kutofahamika haraka hasara iliyotokea, lakini inadaiwa vifaa vilivyoteketea vina gharama kubwa.

Ofisa utawala wa taasisi hiyo, Adamu Mwakalukwa akizungumza na Mwananchi eneo la ajali, leo Jumamosi Oktoba 2, mwaka 2021, amesema ofisi zilizoungua ni maabara tatu za sayansi za kuwafundishia wanafunzi na chumba cha  kompyuta.

Amesema licha ya baadhi ya vifaa kuokolewa, lakini vingi na vyenye gharama kubwa vimeteketea kwa moto huo.

Amesema gharama itafahamika watakapofanya tathmini baadaye.

“Kwa vyovyote vile gharama itakuwa kubwa maana kuna kemikali nyingi  tulizonunua nje ya nchi na ukiangalia kile chumba cha kompyuta nacho kinavifaa vingi vya gharama kubwa, lakini vyote hivyo  vimeteketea na ndizo zinaendesha mtandao wetu wa kompyuta hapa mjini,” amesema Mwakalukwa.

Advertisement

Pia Mwakalukwa amesema hata viumbe hai vya kufundishia walivyovihifadhi kwenye  majokofu navyo vimeteketea sambamba na sampuli za wanafunzi zilizokuwa zimetunzwa kwa muda mrefu.

Kamanda wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji Zanzibar, Rashid Mzee Abdalla amesema wamefanikiwa kuudhibiti moto huo kabla haujaleta madhara makubwa zaidi.

Amesema moto uliuanzia kwenye chumba, kwa mujibu wa mlinzi aliyekuwa analinda eneo hilo ambaye aliwaeleza kuwa alihisi kama kuna shoti ya umeme maana hapakuwa na mtu kwenye chumba hicho.

“Kama hakuna mtu alikuwa anasimamia, labda nyaya zilikuwa mbovu au mfumo wa umeme na kemikali hizo vyote vinaweza kuwa chanzo cha moto huu, bado hatujapata chanzo kamili,” amesema kamanda huyo.

Naye kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Magaharbi, Omar Nassir amesema chumba kilichoteketea kilikuwa kimehifadhiwa vitu vingi vya kitaaluma na wao wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo ni nini.

Na hawana taarifa ya mtu yoyote kujeruhiwa au majengo mengine kudhurika na moto huo.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles