Akiwa ametimiza mwaka mmoja madarakani, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi licha ya kutambua kuwepo minong’ono na watu wanaompinga, ameweka msimamo kuwa hilo halitamzuia kuendelea na mikakati ya kuwaletea Wazanzibari maendeleo aliyoahidi wakati wa kampeni.

Akizungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) katika mahojiano maalumu jana, Ikulu mjini Unguja, Dk Mwinyi aliyeshinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2020, alisema kwa hatua ambazo amekuwa akizichukua dhidi ya watumishi wasioenda na maono yake na hata washindani wake katika siasa, anaamini hataungwa mkono na watu wote.

“Unajua katika uongozi huwezi kuungwa mkono na watu asilimia 100, kuna watu watakupinga. Kuna watu ambao tumeshindana nao kipindi cha uchaguzi tumewashinda, wapo walioridhika wakasema yamekwisha tunasubiri uchaguzi mwingine, lakini wapo ambao bado wana kinyongo,’’ alisema Dk Mwinyi aliyetimiza mwaka mwaka mmoja madarakani Novemba 2, mwaka huu.

mwinyipic

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akijibu maswali ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (kushoto) alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalumu, Ikulu mjini Unguja, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Aliongeza: “Lakini wapo ambao tumewaondoa Serikalini kwa sababu ya mambo ambayo tumeona sio sahihi; mtu kama hawajibiki unamuondoa kama ana viashiria vya rushwa, tunamuondoa; hao pia hawawezi kuunga mkono.’’

Alisema watu wa aina hiyo sio tu hawamkubali, lakini pia wanatumia nguvu kufanya kejeli kuhusu dhana nzima ya uchumi wa bluu, kama sera ya uchumi aliyokuja nayo kwa masilahi ya nchi.

Advertisement

Sitavunjika moyo

Alirudia kauli aliyowahi kuitoa siku za nyuma kuwa havunjiki moyo, kwa kuwa lengo lake ni kuwaletea maendeleo Wazanzibari.

“Dhamira yetu ni kufanya uchumi wa bluu uwanufaishe watu; sitojali nani anasema nini hoja yangu ni kwamba nitaweka nguvu zangu zote katika kuyatekeleza yale yote tuliyoahidi. Nina imani kabisa kwamba yanatekelezeka na ninarudia ndani ya miaka mitano ya kipindi changu nitahakikisha yale yote yanatekelezeka,’’ alisema na kwa uso wa bashasha, aliendelea kusema:

‘‘Maneno yanayojaribu kunivunja moyo wala siyasikilizi; cha msingi ni kusimama imara.

Hali ya uchumi

Pamoja na kuingia madarakani na kisha kukumbana na janga la ugonjwa wa Uviko-19 lililompa wakati mgumu katika ukusanyaji wa mapato, hasa katika sekta mama ya utalii, Dk Mwinyi alieleza kuwa hivi sasa, kwa kiasi kikubwa uchumi umeanza kurudi katika hali yake, kwa kuwa watalii wanakuja kwa wingi na fursa za kiuchumi zinafunguka.

Kuhusu sula la kukuza uchumi na kuboresha huduma za jamii, alisema kuna mwelekeo mzuri kwa sababu mapato ya Serikali yameongezeka, huku fedha zilizokopwa zikifanya yale yote yaliyokusudiwa, hususan katika huduma za jamii, afya, elimu maji na umeme.

“Kwa ujumla nimeridhika na hatua ambazo tumezichukua ndani ya kipindi cha mwaka mmoja; nina hakika tutaweza kuyatekeleza yote ndani ya kipindi kijacho,’’ alisema.

Japo hakutaja takwimu, alisisitiza ahadi yake ya kutoa ajira 300,000 ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, huku akisema ajira hizo ni pamoja na zile za utumishi wa umma, sekta binafsi na wanaojiajiri.

Mustakabali Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Dk Mwinyi alizungumzia pia namna yeye akiwa Rais alivyoshirikiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharrif Hamad kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwa minajili ya kufanya kazi pamoja, jambo ambalo limefanikiwa na kwamba mpaka sasa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja cha kufanya kazi, hajaona dalili zozote za upande mmoja kulalamika.

“Kwa hiyo sasa hivi tunakwenda pamoja na tunakwenda vizuri; sina sababu yoyote ya kufikiria kwamba labda kuna changamoto yoyote inayotokana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.

Awali baada ya kuundwa Serikali hiyo, Dk Mwinyi alimteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kabla ya kufariki dunia na nafasi hiyo kurithiwa na Othman Masoud.

Kuhusu madai kuwa upinzani ulikubali kuingia katika Serikali hiyo ya kitaifa kwa sharti la Serikali yake kufanya uchunguzi kuwabaini watu waliofanya vitendo vya udhalilishaji, ikiwemo kuwapiga watu wakati wa uchaguzi wa 2020, Dk Mwinyi alisema hakukuwa na sharti la aina hiyo.

Alisema SUK ambayo ipo kikatiba imekuwa ikilenga kuondokana na madhara ambayo hutokea kila unapofika uchaguzi.

Aliyataja madhara hayo kuwa na ni pamoja na watu kufikia hatua ya kupoteza maisha, kutalikiana na kutozikana kwa sababu za mitazamo ya kisiasa.

“Watu walikuwa hawazikani kwa sababu ya uchaguzi, wewe chama hiki yule chama hiki, kuna watu walikuwa wanagawana misikiti, wanasema huu msikiti hatusali kwa sababu imamu (kiongozi wa ibada) ni wa chama fulani, haya yote yalikuwa yanatokea,’’ alisema na kuongeza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imelenga kuondoa matatizo hayo.

Aidha, alisema matatizo hayo huwa hayatokei kwa upande wa chama fulani pekee, bali ni athari zinazowafika watu wa pande zote.

“Kwa hiyo kusema kwamba tutaingia katika Serikali mpaka mtuambie mtachukua hatua gani, CCM pia walipata matatizo,’’ alieleza na kuongeza kuwa SUK ina lengo la kuepusha matatizo katika chaguzi zijazo.

“Sawa, yaliyopita yameshapita wala hayajapita katika uchaguzi huu tu, yamepita katika chaguzi nyingi lakini yasijirudie katika chaguzi zingine.”

Kuhusu uchache wa nafasi za uongozi kwa upinzani ndani ya SUK, Dk Mwinyi ambaye katika mazungumzo yake hakusita kumkumbuka Maalim Seif kama mtu aliyekuwa na dhamira ya kuleta amani nchini, alisema:

“Nafasi tatu hazikuja kwa utashi wa mtu bali zipo kikatiba, idadi ya mawaziri ndani ya SUK inategemeana na idadi ya viti vya uwakilishi ulivyoshinda katika baraza la wawakilishi.’’

Alikuwa akimaanisha nafasi tatu ikiwamo ya Makamu wa Kwanza wa Rais inayoshikiliwa na Othman Masoud na mbili za uwaziri zikishikiliwa na Ahmed Nassor Mazrui (Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto); Omar Said Shaban (Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda).

Imeandikwa na

Abeid Poyo, Jesse Mikofu, Mwananchi [email protected]This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles