By Khatimu Naheka

By Ramadhan Elias

KIUNGO wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amehusika katika mabao matatu ya Yanga katika mechi tatu walizocheza hadi sasa na kocha wake Nesreddine Nabi amefichua siri ya nyota huyo kuwa kwenye fomu kwa sasa huku wakongwe wa soka wakishindwa kujizuia na kusema jamaa ni zaidi ya balaa.

Fundi huyo wa mpira amefunga mabao mawili hadi sasa na kuasisti moja katika mechi hizo tatu zilizoifanya Yanga kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama tisa na mabao manne.

Hata hivyo, siri ya uchawi wa Fei Toto wa kuwa kwenye moto imefichuliwa na Kocha Nabi alipozungumza na Mwanaspoti juzi, jijini Dar es Salaam.

Kocha Nabi alisema kabla ya kuanza msimu alikaa na Fei Toto na kumwambia msimu huu anataka kuona makali yake zaidi kutokana na nafasi anayompa.

Nabi, ambaye sasa anampanga Fei Toto nafasi ya kiungo mshambuliaji nyuma ya straika alisema katika nafasi hiyo alimtaka kiungo huyo mbali na kutengeneza nafasi za mabao pia awe bora katika kufunga mabao.

Alisema mabao ambayo Nabi alitaka kuyaona ni ya mashuti makali kutokana na kiungo huyo kuwa na ubora wa kupiga mashuti ambapo anatambua nafasi hiyo ni bora kwake.

Advertisement

“Hamjui kwanini amekuwa bora (Fei Toto) nilipoanza msimu nilikaa naye nikamwambia nataka awe bora msimu huu nitakuwa nampanga namba 10, akiwa hapo awe anarudi kukaba pale kati kazi ambayo anaifanya, pia awe akichezesha timu vizuri,” alisema Nabi na kuongeza;

“Majukumu hayo anayafanya vizuri sababu ni kijana mdogo ambaye ana nguvu ya kujituma lakini pia nikamwambia kufanya hayo pekee haitoshi, nataka pia afunge mabao kwa mashuti. Najua ubora wa Feisal anajua sana kupiga mashuti makali, ila nilimwambia nataka mashuti yanayolenga lango akiweza afunge, naona sasa ameanza kufanya kile ninachotaka.”

Nabi alisema mbali na kumtaka Fei Toto kufanya hayo, ila anajua kwamba katika mashuti hayo yapo ambayo yatapanguliwa na makipa, lakini uwepo wa straika Fiston Mayele utamalizia mipira hiyo.

“Najua yapo mashuti yatakosa kulenga lango, ila yale yatakayopanguliwa na makipa, najua kuna Mayele. Huyu ni mshambuliaji anayejua kukaa maeneo sahihi sioni kama atakosa kumalizia nyavuni na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri,” alisema Nabi aliyeiongoza Yanga pia kubeba Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba Septemba 25.

CHUJI ASHINDWA KUJIZUIA

Ufundi huo wa Fei Toto umemuibua nyota wa zamani wa timu hiyo, Athuman Idd ‘Chuji’, aliyedai kila anapomuangalia kiungo huwa anajiona mwenyewe (Chuji) wa miaka ile akiwa Polisi Dodoma kisha kufanya makubwa Jangwani.

Chuji alisema, Fei anajua namna gani ya kufanya ndani ya eneo lake na kwa wakati sahihi ili kuipatia timu yake matokeo.

“Najiona Chuji kama nimerejea tena uwanjani, kupitia miguu ya Fei, anayafanya niliyokuwa nayafanya nilipokuwa nacheza, anajua sana nini anatakiwa kukifanya na kwa wakati gani,” alisema Chuji na kuongeza tangu alipoondoka uwanjani alikuwa hajamuona kiungo mwenye kufikia kama yeye.

Naye beki wa zamani wa kimataifa nchini aliyewika Reli Moro, Simba na Taifa Stars, Fikiri Magoso alisema kwa wazawa walipo katika Ligi Kuu Bara anamuona Fei mbali zaidi kutokana na uwezo alionao.

Alisema kwa uwezo wake akiendelea kukaza muda si mrefu atasajiliwa na timu za nje kwani uwezo mkubwa anao na anajiamini awapo ndani ya uwanja.

“Fei Toto ndiye kiungo bora mzawa kwa upande wangu mimi, anajua kutekeleza majukumu yake kwa wakati husika, hana mambo mengi kusema kweli anaitendea haki kazi yake. Kiungo mwingine mzawa ninayemuelewa kama Fei Toto ni Mzamiru Yassin, anayecheza Simba, hatajwi sana lakini mambo yake sio mchezo. Naye anajua ni vipi aisaidie timu kwa wakati husika,” alisema Magoso.

Mabao matatu aliyohusika Fei kati ya manne ya Yanga ni sawa na asilimia 75 ya mabao yao.News Source link

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles