By Khatimu Naheka

KOCHA wa Yanga,Nesreddine Nabi amewajia juu mastraika wake akisema kuna kitu amekiona kwa kila mtu kutaka mafanikio binafsi badala ya kuangalia mafanikio ya timu.

Hivyo, amesisitiza kuanzia sasa mchezaji ambaye hatabadilika na kwenda na falsafa ya ushindi ya timu hiyo hatampa nafasi kikosini hata kama awe nani.

Nabi ameliambia Mwanaspoti kwamba timu yake ina ubora sana haswa kwenye mastraika lakini tatizo hilo la kushindwa kucheza kwa ushirikiano na kila mmoja kuwa na papara ya kutaka kufunga yeye ndiyo tatizo ambalo wanalifanyia kazi kwa nguvu na atakuwa mkali sana.

Nabi aliweka wazi amelazimika kuwa mkali baada ya kuona hilo katika mchezo dhidi ya JKU na sasa atafikia uamuzi wa kutompa nafasi mchezaji yoyote atakayeshindwa kushirikiana na wenzake kusaka ushindi kama timu.

“Nimeliona hilo katika mchezo wa JKU na nilikuwa mkali katika vyumba baada ya mchezo kumalizika siku zote inashinda timu anafunga au anatengeneza nafasi mchezaji,” alisema Nabi ambaye anasaidiwa na Cedrick Kaze.

“Tunajua kwamba bado kuna mambo ambayo yanaendelea kujijenga taratibu lakini yapo mazingira ambayo tunapunguza uwezekano wa kutanua ushindi wetu,tunahitaji kuwa na mchezaji anayetambua mahitaji ya timu katika ushindi na sio kuangalia mafanikio yake binafsi,” aliongeza Nabi ambaye ana uraia wa Tunisia na Ubelgiji.

Advertisement

Kocha maarufu kwenye soka la wanawake, Edna Lema ametia neno akisema hatua hiyo inatokana na mzunguko wa nafasi za wachezaji katika timu ambapo kitu muhimu ni mchezaji kuheshimu muda ambao atapewa kucheza na makocha.

“Yanga ina wachezaji wengi bora sasa lazima makocha watafanya mzunguko wa wachezaji kucheza na hilo ndio linalowafanya kutaka kufanya makubwa ili aendelee kupata nafasi ya kucheza,” alisema Lema.

“Kitu muhimu hapa wachezaji wanatakiwa kutambua na kuheshimu muda ambao anacheza uwanjani kocha anatoa nafasi kwa mchezaji ambaye anaweza kusaidia timu na hapo ndipo unapotakiwa ushirikiano kuonekana.

“Makocha wa Yanga wana kazi ya kufanya uwiano wa kikosi kiweze kutengeneza nafasi za kutosha lakini pia itumie nafasi kama kuna wachezaji ambao wataonekana kucheza kwa ushirikiano wa kutosha waendelee kuaminiwa.”

Straika wa zamani wa Yanga na Simba Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ amesema bado Nabi anatakiwa kuendelea kuwakumbusha juu ya ushirikiano mastraika wake kuelewa kwamba anayetoa pasi ya baoa na anayefunga wote wanathamani kubwa.

“Hilo lipo na linaonekana kuna kitu ambacho baadhi ya wachezaji hawaelewi,kwenye timu mchezaji anayetoa pasi ya bao na anayefunga wote wanathamani kubwa mbele ya kocha, kama mchezaji unafika lango la wapinzani ukaona una nafasi finyu ya kufunga mpe mwenzio anayeweza kufunga kirahisi,” alisema Mmachinga.

“Kuna wakati makosa ya namna hii ya wachezaji yanaleta shida kwa makocha wanaonekanba kama makocha hawafanyi vizuri katika ufundishaji lakini kumbe ni suala la wachezaji kujitambua, kwa hiyo nafikiri Nabi anatakiwa kuendelea kuwakumbusha wachezaji wake.”

Ashindilia fiziki

Yanga imeendelea na mazoezi makali na sasa bado wako katika ratiba ya mazoezi ya mara mbili kwa siku wakianzia ufukweni lakini pia jioni wanarudi uwanjani.

Nabi anatambua kwamba wapinzani wao wajao KMC watakuwa imara katika fiziki akianza kuwaandaa mapema na aina hiyo ya ushindani kabla ya mchezo huo wa Oktoba 19 katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

“Mchezo uliopita tulikuwa tunaangalia kile ambacho tumekifanya katika muda wote tuliokuwa kambini lakini tumeendelea na hiyo ratiba tunahitaji kuwa sawasawa kwa mazingira yote ya mchezo,” alisema kocha huyo.News Source link

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles