Wasimamizi wa Ligi ya Kikapu nchini Marekani National Basketball Assosiation ‘NBA’ wametangaza utaratibu maalum wa Afya na Usalama kwa wachezaji juu ya kujikinga na Covid-19 kuelekea msimu mpya wa mwaka 2021-22 unaotaraji kuanza Oktoba 19, 2021 na kumalizika April 2022.

NBA wametoa maelekezo hayo usiku wa jana na kujikita zaidi kwa wachezaji ambao mpaka sasa hawajapata chanjo ya Ugonjwa huo ambao umezidi kuwa tishio nchini marekani kwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 680,000 baada ya visa zaidi ya 42,800,000 kuripotiwa na Shirika la Afya Duniani WHO nchini humo mpaka kufikia jana Septemba 29, 2021.

Taratibu hizo mpya za kujikinga na Covid-19 katika msimu mpya wa NBA 2021-22 ni kama zifuatazo:

1. Wachezaji ambao hawajapata chanjo watafanyiwa vipimo mara nyingi zaidi kuliko wachezaji waliochanja. Watafanyiwa vipimo wakiwa mazoezini, wakisafiri, shughuli nyingine za kitimu na hata kwenye siku za mchezo wenyewe.

2. Hawataruhusiwa kula kwenye chumba kimoja na wachezaji au wahusika wengine waliochanja.

3. Makabati yao ya kuhifadhia nguo na vifaa vyao vya michezo ‘Lockers’ yanapaswa yawe mbali kabisa na wachezaji waliopata chanjo.

4. Kuvaa barakoa na kukaa umbali wa angalau futi 6 na watu waliochanja kwenye kambi ya timu husika.

5. Hawataruhusiwa kutembelea sehemu zenye mikusanyiko pindi wawapo nyumbani kwao. Mfano, Hawatoruhusiwa kwenda Bar, kwenye sehemu za wazi za starehe na mikusanyiko mingine ya burudani.

Licha ya kutoa mapendekezo hayo, lakini mpaka sasa bado NBA inafanya mazungumzo na Chama cha Wachezakikapu wa Kulipwa ‘NBPA’ yaani National Basketball Players Association ili waridhie na kupitisha mapendekezo hayo kabla ya msimu mpya kuanza kwani mpaka sasa inaripotiwa 90% ya wachezaji wamepata chanjo ilhali ni 55% tu ya Wamerakani wote nchini humo waliopata chanjo ya Covid-19.

Baadhi ya wachezaji waliopata chanjo mpaka sasa ni Lebron James, Anthony Davis wa Los Angeles Lakers, Darmian Lillard wa Portland Trail Blazers na Giannis Antetokounmpo wa mabingwa wa Ligi hiyo wa msimu uliopita 2020-2021, Milwaukee Bucks.

Na wale wachezaji baadhi ambao hawajapata chanjo ya Covid-19 ni Bradley Beal wa Washington Wizard na Andrew Wiggins wa Golden State Warriors ambao wamesema ni heri wasalie bila kuchanja. Mbali na taratibu hizo mpya, Lakini inaelezwa kuwa taratibu zilizokuwepo msimu uliopita kama vile kuvaa barakoa na kukaa benchini kwa kuachiana nafasi ya umbali wa mita 2 zitaendelea kama kawaida.

 

Tagged in:

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles