By Luqman Maloto

Dar es Salaam. Uteuzi wa Dk Stergomena Tax kuwa mbunge, unaibua hisia kama ni mwanzo wa Rais Samia Suluhu Hassan kupangua Baraza la Mawaziri.

Dk Stergomena, mwanamke mwenye heshima kubwa kwenye uga wa kidiplomasia, anaingia bungeni kipindi ambacho Taifa halina Waziri wa Ulinzi kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi na Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa alifariki dunia Agosti 2, mwaka huu.

Kwa nafasi hiyo kuwa wazi na kwa uteuzi wake, tafsiri ya moja kwa moja inayojengeka kwa baadhi ya wachambuzi wa mambo ni kuwa Dk Stergomena yupo njiani kwenda kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 55, ibara ndogo ya (4), imeweka sharti la kuwa ili mtu awe na sifa ya kuwa waziri au naibu waziri, anapaswa kwanza kuwa mbunge katika Bunge la Tanzania.

Tayari Dk Stergomena ameapishwa bungeni juzi na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye hakusita kuonyesha furaha yake wakati akimkaribisha mwanadiplomasia huyo.

“Nakupongeza kwa kuteuliwa na Rais katika nafasi zake zile; nichukue fursa hii kukukaribisha na kukupongeza kwa kazi kubwa uliyomaliza kuifanya ya kuwa Katibu Mkuu wa Sadc na tunasikia fahari kubwa, kwani umetujengea heshima na tunasikia fahari kwamba, wewe sasa ni miongoni mwetu. Karibu sana nyumbani,” alisema Spika Ndugai baada ya kumaliza kumwapisha.

Advertisement

Dk Stergomena anakuwa mbunge wa tisa kuteuliwa na rais na hivyo nafasi za uteuzi alizopewa kikatiba kubaki moja.

Dhana nyingine kuwa uteuzi wa Dk Stergomena kuwa mbunge ni mwanzo wa safari ya uwaziri, inajengwa na ukweli kwamba tangu kifo cha Kwandikwa, imechukua muda mrefu kwa Rais Samia kujaza nafasi yake.

Mpaka mwezi uliopita, Dk Stergomena alikuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini ya Afrika (SADC), nafasi aliyoanza kuishikilia tangu mwaka 2013.

Kwa mujibu wa wasifu wa Dk Stergomena, aliyezaliwa mwaka 1960, kabla hajaitumikia SADC kwa miaka nane kama mtendaji mkuu, alikuwa mtumishi wa Serikali kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2008 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Uteuzi wa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki ulikuwa kupanda cheo, kwani kabla ya hapo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.

Stergomena, mama wa watoto wawili, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango mwaka 2006, akitoka kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ubora (BRU), katika Mpango wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Biashara Tanzania (BEST), chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

Alishafanya kazi pia katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamiii (ESRF) kama mratibu na mshauri. Kuanzia Mei 1991 mpaka Aprili 2002, alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Fedha, akiwa mhusika mkuu wa usimamizi wa misaada na uratibu (AMC).

Akiwa Wizara ya Fedha, Dk Stergomena alikuwa ofisa wa usimamizi wa fedha kabla ya mwaka 1993, alipokuwa ofisa mkuu wa dawati la Benki ya Dunia. Mwaka 1995, alikuwa msimamizi mkuu wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Dk Stergomena ni mhitimu wa shahada ya uzamivu (PhD), aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Tsukuba, Japan akiwa amebobea katika maendeleo ya kimataifa.

Awali Stergomena alisoma shahada ya uzamili ya falsafa ya maendeleo ya kimataifa, Chuo Kikuu cha Tsukuba kuanzia Aprili 1995 mpaka Machi 1997. Shahada ya kwanza aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia Julai 1987 hadi Machi 1991.

Januari 1984, Dk Stergomena alijiunga na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dodoma, akichukua diploma ya uongozi wa biashara.

Katika wasifu wake, Stergomena anajipambanua kuwa na ubobezi pia kwenye uongozi, usimamizi wa ufadhili na misaada, vilevile diplomasia na majadiliano ya kimataifa. Amehusika pia kwenye utengenezaji wa mipango hai ya maendeleo Afrika Mashariki na SADC.

Dk Stergomena anaweza kuzungumza lugha tatu kwa umahiri; Kiswahili, Kiingereza na Kijapan. Katika mzunguko wake wa masomo, amepokea mafunzo mbalimbali nchini na nchi tofauti.

Wasemavyo wachambuzi

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Urithi Wangu, Fortunata Temu alisema Rais Samia amefanya uteuzi huo kwa mamlaka aliyonayo na mtu aliyeteuliwa anatosha.

“Kuanzia uzoefu wake na namna alivyofanya kazi nzuri nje ya nchi, ni jambo linalofurahisha na kujivunia kwa mtu aliyefanya vizuri kuthaminiwa ukizingatia kuwa ni mwanamke mwenzangu,” alisema Temu.

Hata hivyo, alisema suala la kumjumuisha au kutomjumuisha katika Baraza la Mawaziri linabaki kwa mwenye mamlaka ambaye ni Rais.

“Ikimpendeza litakuwa ni jambo jema, akiona asiwe ndani ya baraza lake, navyo ni sawa tu kwa kuwa wenye uwezo wa kuwa ndani ya baraza ni wengi,’’ alisema.

Mhadhiri wa siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema anautazama uteuzi huo kuwa ni wa kimkakati ukizingatia uzoefu mkubwa alioupata kwa kufanya kazi na dola huru kadhaa.

“Nafasi yake ilikuwa inahitaji ushawishi wa kufanya kazi na dola huru, pengine baada ya kustaafu Rais Samia ameona uzoefu huo usikae pembeni aende ndani ya Bunge kusukuma ajenda mbalimbali za Serikali,” alisema Dk Mbunda.

Kuhusu uwezekano wa kuteuliwa kuwa waziri, Dk Mbunda alisema kwa sasa ni vigumu kulitabiri hilo, lakini uteuzi wake ungeibua mjadala zaidi iwapo angeteuliwa kuwa mbunge na waziri kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi ya watu.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles