Maafisa wa polisi wa mji wa Minneapolis katika jimbo la Minesota nchini Mrekani wameendelea kupinga vitendo vya afisa wa zamani wa polisi Derek Chauvin aliyemzuia kwa goti George Floyd katika kesi ya mauaji ya Mmarekani huyo mweusi inayoendelea.
Mkufunzi wa mafunzo ya matumizi ya nguvu wa jeshi la polisi la Minneapolis Luteni Johnny Mercil alipanda kizimbani jana wakati wa kusikilizwa kesi ya mauaji ya Floyd katika juhudi za waendesha mashitaka kuikabili na kuifuta hoja kwamba Derek Chauvin alikuwa akifanya alichofundishwa wakati alipombana Floyd kwa goti lake mwezi Mei mwaka uliopita.
Maafisa kadhaa wa polisi akiwemo mkuu wa jeshi la polisi wametoa ushahidi wakisema Floyd hakutakiwa kuzuiwa chini kwa dakika karibu tisa na nusu.
Chauvin mwenye umri wa miaka 45 anakabiliwa na mashitaka mawili ya mauaji na mauaji bila kukusudia ya Floyd mnamo Mei 25 mwaka uliopita.