AfricaSwahili News

Rais Xi: Samia Atafanya Makubwa

 

RAIS wa China, Xi Jinping (pichani) amesema ana imani kubwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atafanya mazuri na makubwa kwa Tanzania kutokana na dhamira yake ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake, Rais John Magufuli.

Xi ambaye ameahidi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais, ametaja kazi ambazo ana imani Samia ataendeleza ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya kimkakati, kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuchukua hatua za kisayansi za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Covid-19.

Balozi wa China aliyemaliza kipindi chake nchini hapa, Wang Ke aliwasilisha salamu hizo za Rais Xi jana alipokwenda kumuaga na kuzungumza na Samia Ikulu, Chamwino jijini Dodoma. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mbarouk Nassor Mbarouk.

Katika salamu hizo, Rais Xi alisema China itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Samia na alimshukuru kwa salamu za heri na pongezi kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kutimiza miaka 100 ambacho pamoja na kufanya mageuzi na kuleta maendeleo makubwa, kimekua kutoka wanachama 50 hadi wanachama milioni 92.

Katika mazungumzo hayo, Samia alimshukuru Balozi Wang kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza uhusiano wa Tanzania 

na China ambao umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na nchi hiyo.

Miradi hiyo ni pamoja na wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo jijini Dar es Salaam na msaada wa Sh bilioni 35 zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Balozi Wang alimshukuru Samia kwa ushirikiano mkubwa aliopata kutoka serikalini wakati wote wa kipindi chake cha Ubalozi. Alisema China ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na covid 19.

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button