By Janeth Joseph

Rombo. Tarafa tatu za Mashati, Usseri na Mengwe wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji baada ya vyanzo vyake vya maji takribani 30 kukauka kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na wananchi kulima kwenye vyanzo vya maji.

Kati ya vyanzo 36 vya maji vilivyopo wilayani humo, vitatu pekee ndio vinazalisha maji kwa asilimia 100 huku vingine vikiwa vimepunguza uzalishaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 80 hali inayosababisha kuwapo kwa mgao mkubwa wa maji.

Wakizungumza na Mwananchi jana Oktoba 13, 2021 kwa nyakati tofauti wananchi wilayani Rombo wameeleza namna wanavyokabiliana na adha kubwa ya maji huku wengine wakilazimika kuamka usiku wa manane kwenda kusaka maji umbali mrefu.

Adolfina Joseph, Mkazi wa Leto wilayani hapa amesema kuwa changamoto hiyo ya maji imekuwa ni ya muda mrefu hali ambayo imekuwa ikiwafanya kushindwa kutekeleza majukumu mengine ya kimaendeleo na kulazimika kusaka maji usiku na mchana.

“Changamoto ya maji hapa Rombo ni ya muda mrefu na tunaoteseka sana ni wanawake na watoto, watu hatulali tunalala tukiwaza kesho yetu itakuwaje ,serikali tunaomba iangalie hili janga kwa jicho la huruma kwasababu tunataabika sana,fikiria wiki inapita maji hatuoni wanasema kuna mgao huu mgao utaisha lini,” amesema Adolfina.

Chrisanta Tesha, Mkazi wa Mengwe amesema kuwa wakati mwingine wanalazimika kuwacha watoto wachanga kitandani na kwenda kusaka maji ambayo upatikanaji wake ni wa shida na wakati mwingine wanalazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji.

Advertisement

“Mtu unaamka asubuhi unatafuta maji kuanzia huo muda hadi mchana tena ndoo moja kichwani, jamani huku Rombo maji yamekuwa ni ya shida mno, maji yamegeuka kuwa almasi, tunateseka. Wanasema kuna mgao wa maji, lakini wiki inapita huoni maji, hii ni changamoto kubwa mno, mamlaka zinazohusika hebu zijaribu kuona namna ya kutusaidia,” amesema Chrisanta.

Akizungumzia changamoto na mgao wa maji wilayani humo, Kaimu Meneja huduma kwa wateja kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira  Rombo, Fidelis Mrosso amesema kuwa kipindi hiki ni cha kiangazi hivyo upatikanaji wa maji ni changamoto kubwa huku akisema asilimia 90 ya vyanzo vya maji vilivyopo vimekauka na kupunguza uzalishaji.

“Kipindi hiki cha kiangazi changamoto ya maji ni kubwa sana kwasababu asilimia 90 ya vyanzo vya maji vimekauka na kupunguza uzalishaji kitu ambacho kinasababisha mgao mkubwa wa maji ambapo tunajitahidi angalau kutoa masaa mawili mawili ya mgao wa maji ili kila mmoja apate kidogo,” alisema Mrosso.

“Vyanzo vilivyopo Sasahivi ambavyo ndio vinavyotoa maji tunategemea vinavyotoka Moshi vijini ambavyo ni vya Whona vilivyopo Marangu na visima vya kuchimba, tuna hali mbaya ya maji kwa sasa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yamepelekea ukame pamoja na changamoto ya watu kulima kwenye vyanzo vya maji,” amesema Mrosso

“Rombo tuna vyanzo 36 vya maji, sita kati yake ni visima vya kuchimba na 30 ni chemchem na maji ya mserereko, kati ya hivi 30 vitatu tuu ndio vinazalisha maji kwa asilimia 100 ambavyo vinahudumia vijiji vitatu tuu,” amesema.

Pamoja na changamoto hiyo amesema tayari serikali imetenga zaidi ya Sh36.9 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Chala kwa ajili ya kuondoa changamoto ya maji wilayani humo.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles