By Luqman Maloto

Taifa la Afrika Kusini limetikiswa na habari ya Nomia Rosemary Ndlovu (46) baada ya kupanga njama na kuua ndugu zake sita, huku akiwa anaandaa vifo vya ndugu wengine, akiwemo mama yake mzazi.

Swali likawa, Rosemary ni nani? Historia yake ikoje? Kwa nini aliua ndugu zake? Wakati viulizo vikiwa vingi, Septemba 14, mwaka huu, Rosemary alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Palm Ridge, Katlehong, Johannesburg na kusomewa mashtaka.

Mwendesha mashtaka wa serikali, Wakili Riana Williams alimsomea mashtaka yake na kumtajia tuhuma za kuua ndugu zake sita. Rosemary kwa kujiamini kupita kiasi, alijibu yote yaliyosemwa ni uongo.

Baada ya kutoka mahakamani, Rosemary alisimama kwa ‘mapozi’ mbele ya wanahabari na kusema: “Nani alijua Rosemary angekuja kuwa mtu maarufu siku moja? Leo niliamka mapema nikajipodoa kwa ‘makeup’ kwa ajili ya kutokelezea kwenye vyombo vya habari.”

Rosemary ni kama hajali kitu, alichosema mahakamani ni kuwa yeye hana hatia na kwamba kama mahakama itamkuta na hatia, basi acha iwe hivyo.

rosemary nyinginepic
Advertisement

Ilibidi jaji anayesikiliza kesi hiyo, Ramarumo Monama, amweleze Rosemary kuwa yeye hana hatia mpaka itakapothibitishwa na mahakama. Akamtaka atoe majibu aliyonayo kadiri ya uelewa wake, ili kuisaidia mahakama.

Tuhuma za Rosemary

Kwa mujibu wa Wakili Riana (mwendesha mashitaka), Rosemary alikodi wauaji wawili ambao walitekeleza vifo vya ndugu zake. Watu hao waliokodishwa kuua ni Lakhiwe Mkhize na Njabulo Kunene.

roseeeepiccc

Taarifa ya Wakili Riana imeeleza kuwa mwaka 2012, Rosemary aliwapa Mkhize na Kunene kazi ya kumuua binamu yake, Witness Madala Homu. Mwaka 2013, ikawa zamu ya dada wa Rosemary, Audrey Samisa Ndlovu. Mwaka 2015, aliyekuwa mpenzi wake, Maurice Mabasa aliuawa.

Inaelezwa zaidi kuwa mwaka 2016, Rosemary aliratibu mauaji ya Zanele Motha, ambaye ni mtoto wa ndugu yake. Mwaka 2017, Rosemary alihusika na kifo cha Mayeni Mashaba, ambaye pia ni mtoto wa ndugu yake. Mwaka 2018, alimuua Brilliant Mashego, ambaye pia ni mtoto wa ndugu yake.

Mwili wa Mabasa (aliyekuwa mpenzi wa Rosemary), ulikutwa na majeraha ya kuchomwa na visu zaidi 80. Kisha, Rosemary baada ya kupeleka madai ya kifo cha Mabasa, alilipwa bima randi 416,000 (zaidi ya Sh64 milioni).

Kwa mujibu wa Wakili Riana, sababu ya Rosemary kutekeleza mauaji hayo ni kujipatia fedha za bima. Na hesabu ya jumla inaonyesha kwamba Rosemary kupitia vifo sita vya ndugu zake, amejipatia zaidi ya randi 1.4 milioni (Sh214 milioni).

Uchambuzi zaidi wa fedha hizo ni kuwa kifo cha Audrey (dada yake), Rosemary alijipatia randi 700,000 (Sh107 milioni). Kwa mauaji ya Zanele Motha, bima walimlipa randi 120,000 (Sh18 milioni).

Ukiacha ndugu sita waliouawa, mashtaka mengine aliyosomewa Rosemary ni kusudio la kula njama za kumuua dada yake mwingine, pamoja na mama yake mzazi, Maria Mushwana.

Hata hivyo, mama yake akitoa ushahidi mahakamani, alisema kuwa upande wake hajui kama mwanawe (Rosemary), alikuwa na njama yoyote ya kukatisha uhai wake, ili ajipatie fedha za bima.

Miongoni mwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ni rekodi za simu za Rosemary, zikionyesha alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na wauaji. Mfano, Januari 28, 2018, alimpigia simu Mkhize mara tano, wakati Januari 30, 2018, simu ya Rosemary iliingia kwa Mkhize mara 10.

Pamoja na ushahidi huo, Rosemary amekanusha kufanya mawasiliano na Mkhize. Akaeleza kuwa simu aliyopiga alijua inamilikiwa na Cebisile Kunene, ambaye ni dada wa Kunene (mmoja wa wauaji). Rosemary alidai Cebisile alimpigia simu kwa namba hiyo ya Kunene, naye akadhani inamilikiwa na dada wa Kunene.

Rosemary ni nani?

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Rosemary alizaliwa mwaka 1975, Tembisa, Afrika Kusini. Mama yake ni Maria Mushwana. Kikazi, alipata kuwa mwajiriwa Jeshi la Polisi, Afrika Kusini.

Rosemary aliwahi kuwa kwenye uhusiano na Maurice, ambaye ni mmoja wa waliouawa. Mapenzi yao yalidumu kwa miaka minne na walifanikiwa kupata mtoto mmoja anayeitwa Makhanani.

Maelezo ya ndani ya familia yake ni kwamba Rosemary amekuwa akitambulika kama mwanachama muhimu. Wanasema kama hadhi ya uanachama ingetolewa kwa madaraja, Rosemary angekuwa mwanachama wa dhahabu kwenye familia yao.

Inaelezwa zaidi kuwa Rosemary amekuwa mtu mwenye msaada mkubwa kwa ndugu zake, aliwachukua wengine na kuishi nao. Mfano, Zanele Motha, alimchukua na kukaa naye kwa upendo mkubwa, ingawa baadaye alikutwa amekufa kando ya barabara, huku mwili ukiwa na majeraha mengi.

Kwa upande wa Rosemary kuhusu kifo cha Zanele Motha, alitoa utetezi akisema: “Nilikuwa naishi naye, lakini alikuwa mlevi sana. Nilijaribu kumwonya aache ulevi uliopitiliza lakini hakunielewa.”

Ukiuelewa utetezi wa Rosemary utapata jawabu kwamba anataka jamii itambue kuwa Zanele Motha alifikwa na mauti kwa sababu ya tabia yake ya kuzidisha kilevi.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Oktoba 14, mwaka huu, mahojiano yatakapoendelea upande wa Wakili Riana (mwendesha mashitaka) na utetezi wa Rosemary.

Itaendelea kesho

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles