By Olipa Assa

TOFAUTI na walivyoanza msimu ndani ya Simba, mawinga, Peter Banda, Ousmane Sakho na Kibu Denis wameonyesha kuwa wao ni bala jipya katika Ligi Kuu Bara kwa namna walivyopindua meza kibabe kutoka kuonekana mzigo hadi kuwa nyota tegemeo kwa sasa.

 Sakho, Kibu na Banda aliyepo kwa sasa kwenye fainali za Afcon 2021 walionekana si mali kitu kutokana na kuanza vibaya huku mzimu wa Clatous Chama na Luis Miquissone waliouzwa mwisho mwa msimu uliopita, wakiwatesa mashabiki wa klabu hiyo.

Hata hivyo, ghafla tu wakali hao wamegeuka vipenzi vya mashabiki kwa aina ya soka wanalopiga na kuanza kuwasahaulisha kina Chama na hasa Sakho ambaye kwenye mechi za Kombe la Mapinduzi amefunika mbovu sawa na Kibu wanaoanza wote kwa pamoja kwa sasa.

Mwanaspoti limezungumza na wadau mbalimbali, walitoa mitazamo yao kuhusu wachezaji hao, namna wanavyoweza wakamaliza kishujaa tofauti na mwanzo wao.

Beki wa zamani wa timu hiyo, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema jambo lililowachanganya mashabiki, walitegemea wachezaji hao wangeanza kwa kishindo ili kuendeleza walichokifanya Luis na Chama.

“Sakho na Banda walikuja kipindi kigumu, walitarajiwa kuziba pengo la Chama na Luis, bahati mbaya miguu yao ilichelewa kutema madini, hapo ndipo mashabiki waliposhindwa kuvumilia,” alisema Bwalya na kuongeza;

Advertisement

“Sakho alianza na majeraha, isingekuwa rahisi kwa kocha kumpanga kikosi cha kwanza wakati anasaka matokeo, ndio maana amewaanzisha Mapinduzi na wameonyesha walichonacho, kitakachompa ujasiri Pablo kumtegemea kikosini.”

Hoja yake iliungwa mkono na mchezaji mwenzake wa zamani, Boniface Pawasa aliyesema tangu mwanzo hakuona ubaya wa kikosi cha Simba na alishauri Banda apewe muda kutokana na umri wake mdogo na Sakho alikuwa majeruhi.

“Sakho, Banda na Kibu walijiunga na Simba wakati ambao wachezaji milii yao ina uchovu wa kucheza mechi nyingi, Sakho akawa majeruhi, Banda umri wake alipaswa azoee ligi, Kibu alikuwa kwenye presha kubwa kutokana na usajili wake, mambo yao yametulia kwa sasa ndio maana wameanza kuonyesha,” alisema Pawasa aliyetamba na Simba na Taifa Stars.News Source link

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles