By Ramadhan Elias

By Daudi Elibahati

MASHABIKI wa Simba kwa sasa wanahesabu saa kabla ya kushuhudia chama lao likishuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kumalizana na Jwaneng Galaxy, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes akiwakomalia mastaa wake ili kumaliza kazi mapema.

Simba itaikaribisha Jwaneng ikiwa ni wiki moja tangu waifumue mabao 2-0 nyumbani kwao mjini Gaborone na tangu warejee nchini kikosi cha mabingwa hao wa nchini wanaendelea kujifua kunoa makali yao kwenye Uwanja wa Boko Veterani, jijini Dar es Salaam.

Mwanaspoti limekuwa likihudhuria mazoezi ya timu hiyo na kuona namna Gomes na vijana wake wakijiweka sawa na kupeana maufundi ya kumaliza kazi mapema kama walivyofanya ugenini, huku kocha huyo akisisitiza hatabadilisha mbinu alizotumia kupata ushindi katika mchezo wa kwanza.

Simba ambayo kwa mara ya mwisho kupoteza mechi ya nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa ilikuwa mwaka 2013, kama italinda ushindi wake huo itatinga makundi na kuwa ni mara ya pili mfululizo kwao, lakini ikiwa ni mara ya nne baada ya kufanya hivyo 2003, 2018 na msimu uliopita huku mara mbili za mwisho ilitinga robo fainali na kukwamishwa na TP Mazembe ya DR Congo na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Katika mazoezi ya jana asubuhi, kocha Gomes na wasaidizi wake watatu, Hitimana Thierry, Milton Nonev na Adel Zrane walionekana kuwakazania vijana wake kukaba zaidi na kutengeneza nafasi za kufunga mabao kuonyesha kuwa Jwaneng kazi wanayo Jumapili Kwa Mkapa.

Kwa dakika 10 mastaa hao walipasha misuli moto chini ya Zrane kisha wakapewa kazi na Gomes aliyesimika vifaa maalumu vyenye umbo kama watu katika maeneo tofauti na kuanza kuelekeza namna ya kukaba kwa nafasi.

Advertisement

Zoezi hilo lilihusisha wachezaji wanne kwa kila midoli miwili huku Gomes akisisitiza spidi na ushapu kwenye kuwahi katika maeneo yenye mpira.

Baada ya hapo aligawa timu ya watu 11 huku ile midoli ikipangwa kivingine tena kwenye eneo la nusu ya uwanja na kuanza kuwaelekeza namna ya kukaba nafasi wakati wapinzani wakiwa na mpira zoezi ambalo lilifanyika kwa ubora mkubwa.

Baada ya kuona vijana wake wameiva kwenye kukaba, Gomes alibadili mbinu na kuanza kuelekeza namna ya kutengeneza mashambulizi na kufunga.

Katika hatua hii aliwachukua viungo washambuliaji, mawinga na washambuliaji ambao alikaa nao kwenye nusu ya uwanja huku wengine waliobaki wakiendelea na programu nyingine chini ya kocha msaidizi Hitimana.

Bwalya, Kibu Denis, Duncan Nyoni, Peter Banda, Jimmyson, Hassan Dilunga, Bernard Morrison, Mhilu, John Bocco na Meddie Kagere ndio walipewa jukumu la kufunga ambapo walipangiwa midoli kama mabeki na kuanza kushambulia kwa pasi za katikati, pembeni na mbele huku Bocco na Kagere wakimtungua kinoma kipa Ally Salim.

Zoezi hilo lilifana kwani mikimbio ya kina Morrison na Dilunga ilikuwa sambamba na pasi za kina Bwalya na Banda na kuwarahisishia kazi Bocco na Kagere ambao walifunga zaidi ya bao 10 kila mmoja kwenye zoezi hilo lililodumu kwa dakika zisizopungua 20.

Baada ya hapo walihamia kwenye kupiga mipira ya kutenga ‘frii-kiki’ ambapo walichaguliwa, Duncan, Bwalya, Zimbwe, Morrison, Mwenda, Nyoni na Lwanga na kupangiwa midoli kama ukuta kisha kuanza kupiga.

Katika zoezi hilo, Duncan, Bwalya, Morrison, Nyoni na Mwenda walifunga sana.

WEMBE ULE ULE

Mapema, kocha Gomes alisema licha ya kushinda mchezo wa kwanza dhidi ya Galaxy bado ameandaa mpango maalumu wa kuendeleza wimbi la ushindi, japo hakutakuwa na badiliko lolote la kimbinu.

“Timu ya ushindi haibadilishwi hivyo sitegemei kubadilisha kikosi.”News Source link

About the Author

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ?Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

View All Articles