Darasa Huru

SIMULIZI | SAMAKI MTU SEASON 3 SEHEMU YA 4


SEHEMU YA NNE
Mfalme alitetemeka kwa hasira,tumbo lake kubwa Kama mama mama mjaamzito mwenye mimba ya watoto mapacha likacheza cheza juu na chini.Hakuamini mtoto mdogo kama Kapirima angekiuka maagizo yake na kuelekea mrima Parmago.Mfalme baada ya kuhakikisha wanakijiji wote wako majumbani isipokuwa nyumbani kwa kina Kapirima,aliamuru nyumba zote zivunjwe.Ameenda mrimani kufanya nini?Au anataka ufalme?Kama anataka ufalme,nani kamwambia maji ya Parmago yatamsaidia?Maswali mengi yalizunguka kichwani kwa mfalme jambo ambalo lilimfanya aamuru nyumba zivunjwe waweze kuingia ndani pengine majibu ya maswali yake yangeweza kujibiwa.Maamuzi yake yalikuwa sahihi,mfalme Katamposhi aliweza kuiona ndoano yenye damu za binadamu zilizokauka,alipoiramba damu iliyoko kwenye ndoano ikiwa imeganda,aliitambua kuwa ni damu ya mama yake mzazi.Mapigo ya moyo wake yakamwenda mbio,hofu yake ikaongezeka maradufu kwani aliweza kugundua kuwa Kapirima aliweza kugundua siri iliyokuwa imejificha.

“Ina maana Kapirima amemnasa mama Baharini?Amemuua au yuko hai?Hapana,ana nguvu nyingi za kumlinda na hawezi kufa kirahisi tena kwa ndoano ndogo kama hii.Nisipochukua maamuzi ya haraka,nitakufa!Lazima niwahi kufanya kitu Kabla wao hawajakifanya,sikutaka kuwaua,lakini inabidi wafe ili niendelee kuwa Salama”Alizungumza peke yake nafsini mwake kisha akacheka cheko zito ambalo liliwafanya askari wake wamshangae kwani hawakujua chochote kilichokuwa kinaendelea.Haraka sana aliwaamuru vijana wake wamfuate,kwa heshima walimfuata na msafara wote ukaelekea kwenye ngome yake.Baada ya kufika kwenye ngome yake,aliingia kwenye chumba chake cha siri na baada ya muda alitoka akiwa na kibuyu kilichojaa maji kutoka mrima Parmago.

“Chukueni mapanga makali Kisha mnifuate!Ardhi yetu imevamiwa na majini wa Baharini,tunapaswa kwenda kuwanasa na hii ndiyo dawa yao.Tunawanasa kiulainiii!Kapirima yeye atafia huko huko msituni,kama atafanikiwa kutoka salama,nitamchinja kwa mikono yangu mwenyewe na mwili wake nitaula nyama.”Alizungumza kwa kejeli,maneno ambayo hayakuwa ya utani kwani ameshakula maiti nyingi za raia wake ikiwemo maiti ya baba yake Kapirima,mzee Kapirima mwenyewe mwaka mmoja uliopita alipokataa Binti yake asiolewe na mfalme huyo katili.Mfalme Katamposhi pamoja na askari wake wakiwa juu ya farasi waliongozana kuelekea Baharini haraka sana,mfalme pekee akiwa anajua ukweli wa kile anachokwenda kukifanya,askari wake aliwadanganya ili kuitunza siri yake.

“Namwaga maji Baharini,watatoka wote Kama binadamu na nitawachinja chinja!Staki upuuzi mimi!Skutaka kuwaua lakini wamenichokoza!”Mfalme Katamposhi Alijisemea peke yake nafsini mwake,dakika kumi zilitosha kufika ufukweni mwa Bahari tulivu ya Mediterania kwa kutumia farasi.Haraka sana mfalme alishuka kwenye farasi wake,aliamuru askari wake kuandaa mapanga yao kushambulia kisha alimimina maji Baharini yaliyokuwa kwenye kibuyu chake alichokitunza kwa miaka mingi.Kisha akatulia kusubili mama yake pamoja na ndugu zake watoke Baharini,uso wake ukiwa umefula kwa hasira.
****


***
Malikia Katamposhi baada ya kufika kwenye makazi yake Baharini,alichukua pete yake nyingine kwani pete ya ulinzi ambayo alikuwa ameivaa kabla hajanaswa na ndoano ya Kapirima,alimpatia ili iweze kumlinda kwenye safari ya hatari aliyomuagiza kwenye mrima Parmago.Pete kama hizo alikuwa nazo nyingi sana na ndiyo urithi pekee alioachiwa na mume wake takribani miaka mia moja ishirini iliyopita baada ya kufariki.Siku anageuzwa kuwa samaki na mtoto wake mwenye uchu wa madaraka,alifanya kila njia na kuhakikisha anafanikiwa kukilinda kibuyu chenye Pete hizo huku watoto wake ambao aligeuzwa nao kuwa samaki na wenyewe kila mmoja akimpatia Pete yake ya kumlinda.

“Pete inakaza!Kuna hatari iko mbele yangu inakuja Baharini.Mungu wangu weeee!Hata Kapirima na yeye yuko hatarini!”Alizungumza kwa hofu,alifahamu kutafsiri ishara ya Pete zake zenye nguvu,baada ya kuvaa Pete iliweza kukibana kidole chake hali ambayo ilisababisha maumi makali.Alipoongeza pete nyingine ya pili kwenye kidole kingine,mambo yalikuwa yaleyale,pete ilikaza sana na kumuumiza.Akiwa anatapatapa hajui nini afanye,aliwakumbuka watoto wake ambao wao pia walikuwa Baharini na walipoteana miaka mingi iliyopita baada ya Bahari kuchafuka na kila mmoja kusombwa na mawimbi kwa upande wake.Alichukua Pete kwenye kibuyu kulingana na idadi ya watoto wake,hapo ndipo nguvu zilimuishia,mwili wake wote ulichoka,matumaini yote yakapotea.Watu wake wote wa Karibu walikuwa hatarini na pete zitakapobana vidole vyake na kupasuka huku vikimsababishia damu kuchuruzika,huo ndiyo ungekuwa mwisho wao.Lakini ghafla,Pete zote ziliregea na kuacha kukaza jambo ambalo lilimfanya atabasamu tena.Kitendo hicho kiliashiria kwamba hatari itatokea lakini haitaweza kumdhuru yeye,Kapirima,wala watoto zake.Malikia akacheka sana kwa furaha.Je,hatari hizo ni zipi?Watapona pona je?Endelea kuwa pamoja na mimi.
*****
Mfalme Katamposhi alisubili sana mama yake pamoja na ndugu zake ambao aliwageuza Samaki waweze kutoka Baharini lakini aliambulia patupu.Dakika zilitoweka,masaa yakatoweka na hatimaye jua liliweza kuzama pasipo ndugu hata mmoja kutokea.Alikichukua kibuyu chake na kukitazama,alikinusa,kilitoa harufu kali.Hakuishia hapo,aliingiza mkono kwenye kibuyu na kuutoa,mkono wake ulitoka ukiwa na minyoo hali ambayo iliashiria maji yalikuwa yameharibika.

“Hakikisha maji hayatoi harufu wala kuchafuka vumbi.Hayo hayataweza kufaa kukutibu,kukulinda wala kufanyia kazi yeyote ile.Maji yenye nguvu ni masafi yasiyo na harufu,hakikisha unayatunza vizuri!”Yalikuwa ni maneno ya mganga wake aliyepoteza maisha miaka mingi iliyopita,maelezo ya mganga ambayo yalimwelekeza namna ya kutunza maji ya mrima Parmago,siku chache baada ya yeye kuwageuza ndugu zake Samaki kwa kutumia maji hayo na Kisha kutwaa Madaraka ya kisiwa Cha Parma.Mganga huyo ndiye miongoni mwa watu aliowaua ili kuifanya siri hiyo kubaki moyoni mwake ili kuulinda ufalme wake.Baada ya kugundua maji hayo hayafai tena,alikasirika sana.Aliwaamuru vijana wake warudi kwenye ngome yao haraka sana huku akitafakari kitu cha kufanya.Hivyo ndivyo malikia Katamposhi pamoja na watoto wake Baharini walipona hatari iliyokuwa mbele yao.Je,Kapirima aliponaje hatari ya kumezwa na mizizi ya ajabu msituni?Tuendelee kuwa pamoja.
***
“….pete hii sio pambo ni ulinzi wako”Alikumbuka maneno ambayo aliambiwa na malikia wake ambaye ni nusu binadamu na nusu Samaki siku moja iliyopita katika ufukwe wa Bahari ya Meditarania.Kwa taabu,akiwa amebakiza sekunde chache tu aweze kupoteza maisha,aliyatamka maneno ambayo yaliifanya mizizi ya mti huo wa ajabu kumuachia huku tayari shingo yake ikiwa imechubuliwa vibaya mno.

“Pe pe pete!pete! ni ni niokoeee!”Bila sauti kutoka,alitamka maneno hayo.Pete aliyokuwa amevaa kwenye mkono wake wa kushoto ilitoa mwanga mkali uliopelekea mizizi iliyomzingira Kapirima kunyauka yote,Kisha mti wote ukakauka na kudondoka chini kitendo ambacho kilipelekea kishindo kikubwa kusikika Kona zote za msitu wa Parmago.Kapirima alikohoa Mara tatu mfululizo,alihema kwa kasi sana ili kuirudisha pumzi iliyokuwa imepotea kwenye mapafu yake,sura yake ilikuwa imebadirika huku macho yake yakiwa yamegeuka na kuwa mekundu.Hilo lilikuwa ni pigo la kitoto lakini lilimnyoosha haswaa,je Itakuaje?Tayari mti ulioanguka umesababisha kishindo ambacho kimeviamsha usingizini viumbe hatari zaidi.

Said Abdullah

Fan of programming| Technology Enthusiast..| System developed|C,C++&java| Junior admin and Publisher of this website

Related Articles

Back to top button
Muhabarishaji News We would like to show you notifications for the latest news and updates.
Dismiss
Allow Notifications

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker