TUZO za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) msimu wa 2020/21, zinatarajiwa kutolewa Oktoba 21, 2021, kwenye ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mpira wa miguu nchini zitatolewa tuzo binafsi 56, ambazo ni tofauti na zile zinazotajwa kwenye kanuni kwa timu washindi wa Ligi mbalimbali.

Kwa muda mrefu Tuzo hizo zilikuwa zikihusisha Ligi Kuu pekee, lakini mwaka huu, TFF imebadili mfumo na sasa zitahusisha pia Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite (SWPL), Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) pamoja na matukio mengine ya mpira wa miguu nchini na zitajulikana kama Tuzo za TFF na zimewekewa vigezo maalum kwa washindi.

Sherehe za Tuzo za TFF, litakuwa tukio la kuzawadia wanamichezo waliofanya vizuri kwenye mashindano yanayoandaliwa na TFF na matukio mengine yenye kuambatana na mpira wa miguu nchini, ambapo Mfumo wa Tuzo za TFF umegawan- yika katika makundi mbalimbali, ikiwemo Tuzo za Kikanuni za mashindano, Tuzo Binafsi za wachezaji na waamuzi.

Pia kutakuwa na Tuzo za kiutawala zikihusisha wasimamizi wa mpira wa miguu na wadau wengine wa mchezo huo hapa nchini, ambapo baadhi ya tuzo hizo ni Tuzo ya Fair Play, Tuzo ya Rais wa TFF, Tuzo ya Mchezaji Gwiji, Tuzo ya Mhamasishaji Bora, Tuzo ya Kamishina Bora na Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja.

Baadhi ya Tuzo zitatolewa kwa mtu zaidi ya mmoja, mfano Tuzo ya Seti Bora ya Waamuzi itatolewa kwa waamuzi wanne na Tuzo ya Kikosi Bora ambayo itatolewa kwa wachezaji 11 wa WPL na pia idadi kama hiyo kwa Kikosi Bora cha Ligi Kuu.