Serikali ya Ujerumani inapanga kuzungumza na Urusi kuhusu kununua dozi za chanjo ya corona ya Sputnik V kama itaidhinishwa na mamlaka za Ulaya. Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn ameiambia redio ya umma ya WDR kuwa Ujerumani imejiandaa kujinunulia kivyake, bila kushirikiana na Umoja wa Ulaya, kama itamaanisha kuwa nchi hiyo itasaidia kuongeza kasi ya kampeni ya kutoa chanjo kwa umma.Â
Spahn amesema Halmashauri Kuu ya Ulaya ilisema jana kuwa haitasaini mikataba ya chanjo ya Sputnik kama ilivyofanya na kampuni nyingine za dawa — kama vile BioNTech.Â
Tangazo hilo la Waziri Spahn limekuja siku moja baada ya jimbo la Ujerumani la Bavaria kusema limesaini barua ya nia ya kununua hadi dozi milioni 2.5 za chanjo ya Sputnik kama itaidhinishwa na Shirika la Madawa la Ulaya – EMA. Ujerumani imeripoti leo zaidi ya maambukizi mapya 20,000 na zaidi ya vifo 300 katika saa 24 zilizopita.