By Mwandishi Wetu

Januari 16 ya mwaka 2016 itabaki kuwa siku yenye kumbukumbu mbaya kuliko zote katika maisha ya Rehema Kibwela (si jina halisi).

Siku hiyo, Rehema (20) alikamatwa na askari polisi wa jijini Arusha aitwaye Raphael Paul, maarufu kama Makongojo ambaye alimpa kipigo kisha kumbaka kwenye uwanja wa mpira wa miguu kabla ya kumlazimisha kunyonya uume wake.

Hivi karibuni, Mahakama ya Rufani imeamuru sehemu ya kesi iliyomfunga Raphael anayetumikia kifungo cha miaka 30 jela isikilizwe upya baada ya kubaini upungufu wa kisheria uliofanywa na mahakama iliyosikiliza kesi hiyo jambo linaloweza kurudisha machungu kwa Rehema.

Kesi ya Raphael ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Iddi Amini jijini Arusha, ni mfano wa jinsi kutozingatia sheria katika uendeshaji mashauri kunavyoweza kuchelewesha kesi za jinai.

Kesi hii inatoa funzo kwa mamalaka kuhakikisha askari wanaoajiriwa kulinda raia na mali zao wanakuwa wenye maadili ya kiwango cha juu ili kujenga imani ya wananchi kwa chombo hicho cha usalala.

Siku ya tukio

Advertisement

Siku hiyo, Rehema ambaye alikuwa mwanafunzi wa sekondari moja wilayani Korogwe, mkoani Tanga alifika Arusha majira ya jioni akiwa njiani kuelekea Korogwe akitokea nyumbani kwao, Mwanza.

Asijue yatakayompata, Rehema alishuka Arusha akitumaini kulala kwa binamu yake (jina linahifadhiwa) ili siku inayofuata apande basi la kuelekea Korogwe.

Kwa bahati mbaya hakumkuta kwani alikuwa amehama kwenye nyumba aliyokuwa anaishi hivyo akalazimika asake mbadala wa sehemu ya kulala.

Aliamua kumtafuta rafiki yake Sakina Mketo (si jina halisi) aliyekuwa anaishi Kwa Mrombo lakini kabla ya kwenda huko, alipitia stendi kukata tiketi ya basi asubuhi safari ya Korogwe.

Baada ya kukata tiketi, Rehema alielekea Kwa Mrombo na kufika huko saa mbili usiku na kuanza kumtafuta Sakina kwa simu yake ya mkononi. Aliendelea kumtafua na kuongea na watu wengine hadi simu yake ikaishiwa muda wa maongezi kukwama kuendelea na suala hilo, asijue la kufanya.

Akiwa ameanza kupata wasiwasi, Rehema alifanya kila jitihada kufika nyumba aliyoishi Sakina bila mafanikio kwani alipotea licha ya ukweli kwamba aliwahi kutembelea nyumba hiyo mwaka 2014.

Rehema alianza kuingiwa na wasiwasi kadiri muda ulivyokwenda na kuamua kwenda eneo la kituo cha mabasi kujihifadhi akiamini atakuwa salama zaidi. Akiwa njiani alikutana na mtu aitwaye Stephen Richard ambaye alipata shauku ya kujua kwa nini binti huyo alionekana kuhamanika baada ya kumkuta akitangatanga eneo hilo.

Rehema alimsimulia yaliyomsibu. Stephen, kwa kutumia simu yake, alifanya kila jitihada kumpata Sakina ambaye simu yaki iliita bila kupokelewa.

Wakati Rehema na Stephen wakifanya kila jitihada za kutafuta makazi ya Sakina, ambayo kwa mujibu wa Rehema yalikuwa karibu na kituo cha mafuta na uwanjwa wa mpira uliokuwa karibu na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ghafla alijitokeza mtu aliyejitambulisha kuwa ni askari polisi.

Raphael alianza kwa kuhoji kama Rehema na Stephen walikuwa wakijuana na baada ya kujua kuwa walikuwa hawajuani, askari huyo alimzaba kofi Stephen na kuwaamuru waondoke nae kuelekea kituo cha polisi.

Kila Rehema alipohoji kwa nini alikuwa akiwapeleka kituoni, askari huyo aliwapiga huku akiwasukuma huku na kule akidai kuwapeleka kituo cha polisi.

Kwa bahati, watu waliokuwa wakipita eneo hilo walionekana kumfahamu vizuri askari huyo ambaye baadhi ya watu walimtambua kwa jina la Iddi Amini. Baada ya muda mfupi, askari huyo alimwamuru Stephen kuondoka na yeye kubaki na Rehema huku akiwa amemshika mkono.

Mwanzoni, Rehema alimsihi askari huyo amwachie lakini alikataa katakata na kuendelea kumshikilia mkono na kusisitiza kuwa yeye ni askari polisi huku akimwonyesha kitambulisho chake.

Baada ya kuona kile kitambulisho cha uaskari, Rehema hakuwa na namna isipokuwa kuamini alikuwa katika mikono salama.

Kilichofuata ni Raphael kumwelekeza binti huyo amfuate kituo cha polisi kwa maelezo kuwa atapata muda mzuri wa kumtafuta rafiki yake Sakina.

Akiwa bado amemshika mkono, Raphael alitembea mwendo mfupi na Rehema na kufika kwenye uwanja wa mpira. Rehema alipojaribu kuhoji kwa nini alikuwa akimpitisha eneo lisilo na watu na lenye giza nene na kukwepa njia nzuri upande mwingine, Raphael alimjibu kwa ukali ‘funga mdomo wako malaya wewe.’

Akiwa amejaa hofu, na asijue la kufanya, Rehema alianza kulia kwa sauti. Wakati huo tayari walikuwa katikati ya uwanja wa mpira hivyo sauti yake ya kuomba msaada haikufika mbali, waliko watu.

Hapo ndipo Raphael alipomsukuma Rehema mpaka huku akimtishia kipigo endapo atathubutu kupiga kelele.

Rehema aliendelea kupiga kelele kuomba msaada, hata hivyo, hazikufika mbali. Hakuna aliyefika kumsaidia hivyo kumfanya askari huyo afanikiwe kulala kifuani kwake huku akimnyonga shingo.

Kwa ujasiri wake, Rehema aliendelea kupambana na kupiga kelele kitendo kilichozidi kumkera askari huyo aliyeamua kumzaba tena kibao na kuanza kumpiga bila huruma hadi alipoishiwa nguvu na baadae kupoteza fahamu.

Hapo Raphael alimvua nguo binti yule na kumwingilia kwa nguvu. Baada ya kupata fahamu, Rehema alijikuta uchi na kugundua tayari alikuwa amekwishabakwa. Alikuwa akihisi maumivu makali sehemu za siri huku mbegu za kiume zikitoka sehemu hiyo.

Kabla ya kufanyiwa unyama huo, Rehema alikuwa bikra. Wakati huo Raphael alikuwa akipekua begi la Rehema na baada ya hapo alimfuata tena. Zamu hii alimwamuru anyonye uume wake.

Akiwa na woga wa kipigo, Rehema alikubali kunyonya uume wa askari huyo. Alipochoka na akiwa amekata tamaa kufanyiwa unyama ule, Rehema aliung’ata kwa nguvu uume wa Raphael.

Kitendo hicho kilimuudhi Raphael ambaye sasa aliamua kumpa Rehema kipigo kikali huku akilalamika ‘unataka kunifanya hanisi!’

“Sasa nitakufanya tasa,” Raphael alimwambia na kuanza kuingiza vidole vyake katika sehemu za siri za Rehema kwa lengo la kuharibu mji wa mimba kitendo ambacho kilimsababishia Rehema maumivu makali.

Raphael aliendelea kumpiga kisha akachukua Sh177,000 na chupa ya manukato iliyokuwa katika begi mwanafunzi huyo.

Baadaye alimkojolea Rehema sehemu zake za siri na sehemu nyingine za mwili, ngua zake zilizokuwa kwenye begi kisha akaondoka. Kabla ya kuondoka alimtishia kuwa atawaleta majambazi wamuue.

Baada ya Raphael kuondoka, Rehema alivaa nguo zake akiwa na maumivu makali na kujikokota mpaka kwenye kituo cha mafuta kilichokuwa karibu. Hapo alimsimulia mhudumu mwanamke wa kituo hicho, yote yaliyomsibu, tangu akiwasili Arusha hadi alipofanyiwa unyama.

Pia alimtaja na kumwelezea mlinzi wa kituo hicho cha mafuta mwonekano wa askari aliyembaka. Mwanzoni, hawakuyaaminika maelezo yake lakini baada ya kuona kitambulisho chake cha shule na tiketi ya basi, walimwamini.

Hapo mhudumu huyo aliamua kumjulisha baba yake Rehema (jina linahifadhiwa) kuhusu madhira yaliyompata mwanaye halafu akampa Rehema sehemu ya kupumzika kwa kuwa ilikuwa ni saa tisa usiku.

Baadaye Rehema alisindikizwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na na mhudumu huyo pamoja na mlinzi wa kituo hicho cha mafuta alikosimulia yaliyomsibu na jinsi anavyomfahamu Raphael ambaye alikaa naye kwa zaidi ya saa saba kuanzia saa mbili usiku.

Aliuelezea mwili, rangi na jina lake. Alielezea pia kuwa aliung’ata uume wa askari huyo na kumwumiza. Alieleza alilitambua jina lake kupitia kitambulisho alichowaonyesha wakati akiwakamata.

Rehema alipewa fomu ya matibabu (PF3) na kupelekwa hospitali ya Mount Meru ambako alilazwa kwa siku 10.

Mbakaji atambuliwa

Siku hiyohiyo (Januari 17 mwaka 2016), Inspekta Msaidizi wa Polisi, Mahita Omar alielekezwa kuandaa gwaride la utambulisho ili Rehema apite kumtambua mbakaji wake kama alikuwepo.

Rehema alimtambua Raphael na kumwonyesha kwa kidole kuwa ndiye aliyembaka…

Itaendelea Kesho

…kujua jinsi Raphael alivyokamatwa, kushtakiwa na kufungwa miaka 30 jela. Jinsi alivyopoteza rufaa yake ya kwanza Mahakama Kuu na uamuzi wa hivi karibuni ulioamuru kesi hiyo isikilizwe upya.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles