Advertisement Scroll To Keep Reading
Swahili News

Unyama wanaofanyiwa madereva wa malori

Advertisement Scroll To Keep Reading

Dar es Salaam. Madereva wa malori nchini wamelalamikia hali ya usalama wao katika nchi jirani za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) wakiitaka Serikali iingilie kati kukomesha “unyama” wanaodai kutendewa.

Advertisement Scroll To Keep Reading

Madereva hao kupitia Chama cha Madereva wa Malori Tanzania (TADWU) wanadai kuteswa hadi kupata majeraha, baadhi yao kupoteza maisha baada ya kutekwa na wengine kunyanyaswa na askari wa nchi wanakopeleka au kuchukua mizigo.

Hata hivyo, Serikali kupitia Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Hassan Yahya imesema malalamiko ya matukio ya ukatili kwa madereva imekuwa ikiyashughulikia kila wanapopata taarifa.

Related Articles

“Ni kweli matukio hayo yapo, lakini ukilinganisha na idadi ya malori zaidi ya 10,000 yanayofanya safari za Tanzania Zambia na DR Congo kwa siku, matukio si mengi sana,” alisema Balozi Yahya.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho alisema hajapata malalamiko rasmi ya chama cha madereva.
“Wao wana chama chao na ndiyo kazi yao kuwasilisha changamoto zao, basi wazilete wizarani,” alisema Dk Chamuriho.

Kilio cha madereva

Advertisement

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tadwu, Schubert Mbakizao alisema kumekuwa na matukio mengi ya kutekwa na kuporwa mizigo, akitaja mikasa minne ya madereva waliokuwa wamebeba madini ya shaba kutoka Zambia kupeleka Dar es Salaam, kufanyiwa vitendo vya ukatili na watekaji.

“Miongoni mwa vitendo hivyo, madereva hupuliziwa dawa ya mbu, pilipili au kupigwa baruti na kuzimia kisha kutupwa msituni.

Baada ya matukio hayo, gari huchukuliwa na watekaji na kwenda kushusha mzigo huku dereva akipatikana baadaye akiwa hajitambui.

“Wapo madereva wawili (anawataja kwa majina) walitekwa walipokuwa wakitokea Congo. Hii imekuwa kawaida kabisa hata wenye kampuni wanajua,” alisema Mbakizao.

“Tumelalamika muda mrefu sana lakini hakuna mabadiliko wala hatua zozote ambazo zimechukuliwa mpaka sasa. Kuna wakati tulifikia hatua ya kupanga mgomo ili hatua zichukuliwe,” alisema.

Alisema baadhi ya madereva waliotekwa na kuachwa hawajitambui, walipatikana baadaye magerezani nchini Zambia wakituhumiwa kuiba mizigo.

“Kinachotushangaza ni gari kutekwa ikiwa na ulinzi wa kampuni iliyopewa jukumu hilo katika nchi husika.

“Msindikizaji anakuwa na nyaraka zote za mzigo anampangia dereva sehemu ya kula, kusimama na mahali pa kulala. Msindikizaji anaweza kutoa amri ya kusimamisha gari hata kama dereva anaona hakuna usalama.

“Hata kama dereva anashauri hapa si sehemu salama, mlinzi anaweza kukutisha kuwa atatuma taarifa ofisini kwako na magari yenu yazuiwe kupakia mzigo. Kwa kuwa matajiri wetu wanapenda biashara, wanasema wewe msikilize msindikizaji,” anasimulia.

Mbakizao alisema kitendo cha kumsikiliza msindikizaji huyo ni kujiingiza mtegoni.

“…Msindikizaji akishamaliza shughuli zake anakuja na watu wengine kama vile wamemteka, wanakuwekea baruti shingoni na kupiga shoti, unapoteza fahamu.

“Ukija kupata fahamu unajikuta mikononi mwa polisi na gari halipo na likija kupatikana halina mzigo. Ajabu dereva anapelekwa magereza lakini msindikizaji aliyekuwa na nyaraka haunganishwi na huwezi kujua yuko wapi,” alidai Mbakizao.

Mbakizao alisema mizigo inayolengwa zaidi ni shaba kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam, lakini inayokwenda Afrika Kusini hawasikii ikiguswa na watekaji wala madereva kufanyiwa unyama huo.

“Imefikia wakati sasa hata askari ambaye huwa anatusaidia ametuchoka. Hata Mkuu wa Polisi aliyeondoka hivi karibuni Zambia alifanya kikao nasi akatuahidi neema, lakini hakuna kilichobadilika,” alisema.

Uongozi wa Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa) umekiri kuyajua malalamiko ya madereva na kuwa wamekuwa wakiyawasilisha serikalini.

“Tunayashughulikia kwa njia mbili, kwanza tumeshawasilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na pia kule Zambia kuna kamati ya pamoja inayokutana mara nne kwa mwaka,” alisema msemaji wa Tatoa.

This article Belongs to

News Source link

Advertisement Scroll To Keep Reading

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

Related Articles

Back to top button

AdBlock Detected

If you enjoy our content, Please support our site by disabling your adblocker. We depend on ad revenue to keep creating quality content for you to enjoy for free.