By Hadija Jumanne

Wakati wakulima wengi wakipata wasiwasi kwa kukosa mvua, wale wanaofanya umwagiliaji katika Bonde la Ziwa Victoria bado wanalia na athari za janga la Uviko-19.

Licha ya kuyanufaisha mataifa mengine ya Afrika Mashariki huku likiwa chanzo kikuu cha mto Nile unaoenda mpaka nchini Misri, Bonde la Ziwa Victoria ni muhimu nchini, hasa katika mikoa minane inayolizunguka ambayo ni Mwanza, Mara, Arusha, Kagera, Simiyu, Geita, Tabora na Shinyanga.

Kaimu Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Jiji la Mwanza, Salome Nzingula anasema mkoa huo una wakulima 507 wanaomwagilia, hasa katika kata za Lwanhima, Buhongwa, kingo za Mto Nyashishi, Luchelele na mwambao wa Ziwa Victoria.

Pius Budodi (51), mkulima katika Kata ya Lwanhima wilayani Nyamagana anasema kuanzia Machi 2020, korona ilipothibitika nchini, wanunuzi walipungua kwa kuhofia kuambukizwa, hali iliyowaacha bila kipato cha uhakika.

“Wanunuzi wanaofuata mbogamboga katika Soko la Buhongwa tunakouza walipungua. Biashara ilishuka kwa kasi ndani ya miezi sita, kuanzia Machi hadi Septemba 2020,” anasema.

Kabla ya janga hilo, anasema ndoo moja kubwa ya nyanya walikuwa wanaiuza kwa Sh30,000, lakini Uviko-19 uliishusha bei hiyo mpaka Sh8,000, ingawa sasa hali imerudi kama zamani, kabla ya janga hilo kutokea.

Advertisement

Budodi, baba wa watoto saba aliyeanza kilimo mwaka 1991, ni mmoja wa zaidi ya wakulima 200 wanaofanya umwagiliaji mwambao wa Ziwa Victoria wakilima zaidi mbogamboga na matunda.

Msengi Magari (61), mkulima mwingine, anasema janga la korona lilishusha kipato chao na athari zake bado zinadumu hata sasa. Msengi, aliyestaafu Jeshi la Polisi mwaka 2014 baada ya kulitumikia tangu mwaka 1982, anafanya shughuli zake katika eneo la Zahanati wilayani Ilemela.

Akilima zaidi mchicha, mtama, mikunde, majani ya maboga na matembele, anasema alikuwa anauza kati ya Sh80,000 hadi Sh100,000 kwa siku, lakini janga hilo lilishusha mapato yake mpaka Sh40,000, hivyo kumvurugia mtiririko wa kipato.

“Wateja huja kununua kwa bei ya jumla na kwenda kuuza Soko la Kirumba. Kilimo hiki kimeniwezesha kujenga nyumba ya kisasa mjini Ilemela, kumiliki mifugo na kununua jenereta ninalolitumia katika za umwagiliaji,” anasema.

Ester Anthony (41), mkulima na mkazi wa Bugarika anasema kipindi cha Uviko-19 kiliwapa changamoto, kwani kuna wakati hawakupata kabisa wateja.

“Siku nyingine tulikuwa hatuuzi mpaka ikabidi nipeleke mboga zangu sokoni Kirumba kulikokuwa na wanunuzi wachache. Wakati mwingine mboga zilikuwa zinalala, ilikuwa hasara,” anasema Ester.

Mfanyabiashara wa mbogamboga katika Soko la Kirumba na Buhongwa, Elina Ntantu (59) anasema hali ilikuwa mbaya, ingawa sasa biashara imeanza kuimarika baada ya watu wengi kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Kaimu Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Jiji la Mwanza, Salome anasema korona iliathiri sekta nyingi za uchumi, wakiwamo wakulima.

“Serikali ipo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Tumekuwa tukiwakutanisha wakulima katika vikundi ili wakopeshwe sehemu ya asilimia 10 ya fedha za halmashauri,” anasema Salome.

Vilevile, anasema wanawapa taarifa na elimu juu ya mabadiliko ya tabianchi wajue namna na wakati wa kulima.

Taarifa za Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zinaonyesha mwaka 202/21, Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilitoa mikopo ya Sh1.3 bilioni kwa vikundi vya wananchi.

Halmashauri nyingine za mkoa huo nazo zilitenga fedha zilizowanufaisha wananchi. Ilemela ilitoa Sh1 bilioni, Misungwi ilikopesha Sh160 milioni na Magu Sh231 milioni, bila kusahau Kwimba iliyokopesha Sh191 milioni.

Mamlaka Bonde la Ziwa Victoria

Ofisa Habari wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria, Perpetua Masaga anasema Uviko-19 kuathiri watumiaji wa maji kulishusha mapato yao pia. Mamlaka ya bonde hilo ndiyo inayotoa vibali vya matumizi ya maji.

Takwimu zilizopo zinaonyesha hadi Novemba 2021, Tanzania ilikuwa na watu 26,164 waliougua korona, huku 725 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

“Ugonjwa wa korona umewakumba watumiaji wa maji ambao ni wateja wetu, hivyo wanachelewa kulipa bili kwa wakati kwa kutozalisha. Wengine wanafunga biashara zao,” anasema Perpetua.

Bodi hiyo anasema imetoa vibali vya matumizi ya maji zaidi ya 900 kwa mamlaka za maji, viwanda vikiwamo vya kusindika samaki pamoja na Kiwanda cha Sukari Kagera.

“Tunaendesha bodi kwa kutumia bili za maji, kwa sababu tunatoa vibali vya maji na wananchi wanachukua maji kwa ajili ya uzalishaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, sasa uzalishaji ukiathirika iwe kiwandani, hotelini au katika kilimo, basi mapato ya bodi yataathirika,” anasema Perpetua.

Makala hii imeandaliwa kwa udhamini wa taasisi ya InfoNile.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles