AfricaSwahili News

Vyuo Vikuu Wampongeza Samia Tozo Za Miamala, Mikopo

 

JUMUIYA ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyochukua hatua kutatua changamoto za wananchi na wanafunzi ikiwamo kuingikia kati tozo za miamala ya simu na kuondoa tozo ya asilimia sita katika mikopo ya wanafunzi.

Aidha, wameiomba Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuharakisha wiki hii kutoa fedha kwa wanafunzi wa vyuo walioanza mafunzo kwa vitendo ili wasikwame kutekeleza hatua hiyo muhimu kielimu.

Katika hatua nyingine, Tahliso imeandika andiko lisilo la wazi kwa HESLB kuimba serikali mwaka huu kila mwanafunzi atakayeomba mkopo apewe bila kujali shule za sekondari alizosoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tahliso, Frank Nkinda alisema serikali imekuwa sikivu katika kushughulikia matatizo ya wananchi wakiwemo wanafunzi na kumpongeza Rais Samia kwa namna alivyoingilia kati suala la tozo la miamala ya simu.

“Maamuzi ya Rais ni ya kuonesha ameguswa na hili. Nia ya serikali kwa tozo haikuwa mbaya, ila hali halisi ya Watanzania jambo hili lingetuumiza wengi za sisi wanafunzi na wahitimu tukiwepo, tunampongeza Rais Samia kwa kuliona hili,” alisema Nkinda.

Katika sherehe za wafanyakazi Mei Mosi mwaka huu, Rais Samia alifuta Tozo la Kutunza Thamani ya Fedha (VRF) kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

“Tunamshukuru na kumpongeza pia kwa kuondoa asilimia sita ya mikopo. Mungu ametupa Rais msikivu kuondoa tozo hii ilikuwa mwiba kwa wahitimu wanufaika wa mikopo,” alisema Nkinda.

Alisema wanavyuo wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo baadhi zinaendelea kupitiwa majawabu ikiwemo ya tozo ya asilimia sita na kutengewa kiasi kikubwa cha fedha mwaka huu cha Sh bilioni 570 kwa ajili ya mikopo.

Aliwahakikishia wanafunzi kuwa jumuiya hiyo itaendelea kufuatilia changamoto zao na kuchukua hatua kwa mujibu wa utaratibu uliopo kuzipatia majibu.

Kuhusu mafunzo kwa vitendo, aliiomba HESLB kuharakisha upatikanaji wa fedha hizo wiki hii kwa kuwa tayari kuanzia juzi Jumatatu, wanafunzi wameanza mafunzo hayo bila fedha hiyo na wengine wataanza kesho Alhamisi.

Akijibu maswali kuhusu wanufaika wa mikopo waliosoma shule binafsi za kimataifa na za mkondo wa Kiingereza kutopatiwa mikopo kwa kukosa sifa kwa sababu ya kusoma shule hizo, Nkinda alisema wameandika andiko lisilo la wazi kwa bodi kuishauri serikali kuhusu hilo.

“Tunaamini mwaka huu 2021/2022 watakaoomba watapata mikopo. Niwaombe wanafunzi wote wanaoona wana uhitaji waombe kwa kufuata taratibu na akipata changamoto aende chuo chake kuna msaada ataupata wa kutatua tatizo lake,” alisema Nkinda.

Naye Kamishna wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii, Abdallah Abdallah, aliipongeza serikali kwa kuongeza nafasi kwa wenye mahitaji maalumu na kuweka sera inayolazimisha waajiri kuajiri watu hao kwa asilimia tatu.

Aliiomba iendelee kuboresha miundombinu ya vyuo kwa wenye mahitaji maalumu ili kuwawezesha kusoma bila shida na kufikia malengo yao.

Kwa upande wake, Katibu wa Tahiliso, Janeth Gasarasi aliwakumbusha wanafunzi na wananchi wote kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) kwa kufuata miongozo ya wataalamu wa afya.

Juzi Rais aliagiza mawaziri wakae na kupitia upya tozo za miamala ya simu baada ya kuwepo malalamiko mengi. Tozo hizo mtu akitoa kwa wakala sh 50,000 anakatwa 4,700 badala ya 2,400 ya awali kabla ya makato hayo ya kodi ya serikali yaliopitishwa kisheria na Bunge mwaka huu.

Dr john Masawe

Medical Laboratory Scientist (MLS) |Dancer|Software Developer|Multitalented|??|Entrepreneur|Researcher ? Founder, CEO, Admin and Publisher Of This Website

Related Articles

Back to top button

AdBlock Detected

If you enjoy our content, Please support our site by disabling your adblocker. We depend on ad revenue to keep creating quality content for you to enjoy for free.