Wachimbaji madini wawili wa Kichina wameripotiwa kutekwa nyara kwa ajili ya fidia katika jimbo la Osun nchini Nigeria.
Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya kitaifa, watu wasiojulikana walishambulia mgodi wa dhahabu ulioko katika kijijini cha Okepa/Itikan, viungani mwa jimbo la Osun.
Wachimbaji madini wawili wa Kichina walitekwa nyara kwenye shambulizi hilo, na walinzi wawili waliokuwa katika mgodi huo wa dhahabu pia walijeruhiwa.
Viongozi wa mamlaka walisema kwamba vikosi vya usalama vilitumwa mkoani humo na kuanzisha operesheni ya kuwasaka watekaji nyara.
Miezi miwili iliyopita, Wachina watatu walitekwa nyara na mlinzi mmoja akauawa kwenye shambulizi lililotekelezwa na watu wenye silaha katika jimbo la Osun.
Ingawa adhabu ya utekaji nyara wa fidia ni hukumu ya kifo katika majimbo mengi ya Nigeria, visa kama hivyo vimeshindwa kuzuiwa.