By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Je! Wewe ni mzazi au mlezi, unampa mwanao simu achezee? Acha kuanzia sasa, kwani wataalamu wa afya ya macho wametaja athari ambazo mtoto anaweza kuzipata akitumia simu hasa walio chini ya umri wa miaka miwili.

Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya macho na leo ikiwa kilele cha siku hiyo, wataalamu wamesema mwanga wa buluu utokao katika kioo cha simu una athari za moja kwa moja kwa mtoto chini ya miaka miwili iwapo atakitumia kifaa hicho.

Mwanga huo wa buluu umetajwa kuwa na nguvu inayoathiri sehemu za ndani ya macho zinazofanya kazi katika kuona pamoja na kusababisha kemikali zinazolinda jicho ‘Alpha tocopheryl’ kushindwa kujitengeneza.

Hayo yamezungumzwa na daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya Aga Khan, Tawakali Mtanda mapema wiki hii katika mahojiano maalum na Mwananchi.

Amesema tofauti kubwa ya macho ya mtoto na mtu mzima ni kwamba macho ya mtoto bado hayajapata uwezo wa kuzuia mwanga wowote utakaoathiri macho.

Advertisement

“Ningeshauri sana hivi vifaa visitumike kwa watoto Mara nyingi wazazi wana tabia mtoto akisumbua anampa simu hususani kwa watoto wa chini ya miaka miwili ile miale inaathiri macho yao mapema sana.

“Baadaye itakuja kumletea matatizo makubwa, ingawaje inachukuliwa kawaida lakini kila wakati ambao mtoto anashika ile simu anazidi kuyaangamiza macho yake,” ameeleza na kuongeza;

“Kwa sababu kwa watoto hususani kuanzia miaka 0 anapozaliwa mpaka anapofika miaka 7, huu ni umri ambao mtoto anakua. Kabla ya miaka miwili mtoto ana vitu anavyoviangalia anavitambua kwa hiyo itamjengea tabia ya kupenda kuviangalia hivyo vitu mara kwa mara kwa hiyo tunavyomuingiza mtoto katika mwangaza ule mkali inamnyima fursa ya kuona vitu vingine vikiwa katika umbali,” amesema.

Dk Mtanda amesema kumpa mtoto chini ya miaka miwili simu pia kunamnyima fursa ya kuchangamsha ubongo wake kwa kuvumbua vitu vingine.

Wakati simu zikitumika mpaka maeneo ya vijijini na hivyo kumfanya kila Mtanzania kumiliki kifaa hicho, Dk Mtanda anasema haijalishi ni simu ya aina gani, bali mwangaza unaotoka katika kifaa hicho ni wa bluu kitaalamu unaitwa ‘blue light’.

“Hii blue radiation ni mwanga ambao ni mkali sana, ukiangalia katika mfumo wa mwangaza unakuta mwanga wa kijani, mwekundu na njano hauna nguvu  kama huu mwangaza wa rangi ya bluu, athari yake ni kubwa baada ya muda huweza kuleta tatizo la upofu, kuna ugonjwa ambao unaitwa ‘macular degeneration’ sehemu ya katikati ya jicho inakuwa inaathirika hususan unawatokea wazee.

“Lakini imetabiriwa katika miaka inayofuata 10 hadi 20 baadaye wagonjwa wengi watakuwa ni vijana kutokana na huu mwanga wa bluu ambao unaathiri sehemu za ndani ya macho zinazofanya kazi katika kuona,” amesema Dk Mtanda.

Naye Profesa Li Li, kiongozi wa hospitali ya macho huko Singapore amesema mionzi ya simu inayoingia ya moja kwa moja kwenye macho kwa zaidi ya dakika 30 na kuendelea inaweza kusababisha mpangilio na mabadiliko wa seli macho na hivyo kusababisha saratani na kushindwa kuona kabisa.

This article Belongs to

News Source link

About the Author

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website

View All Articles